Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akisalimiana na uongozi wa Kijiji cha Matumaini alipokitembelea kituo hicho jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akiwa amembeba mmoja wa watoto wanaolelewa katika kijiji cha Matumaini alipowasili kituoni hapo, jijini Dodoma.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe. Mwanaidi Ali Khamis akitoa zawadi ya sikukuu ya Eid El Fitri kwa watoto wa kijiji cha Matumaini alipotembelea kituoni hapo Jijini Dodoma.
Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW
…………………………………………………………………………………
Na Mwandishi Wetu Dodoma
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anayeshughulikia masuala ya Maendeleo ya Jamii, Mwanaidi Ali Khamis ametoa wito kwa jamii kushirikiana katika malezi ya watoto wanaoishi katika mazingira magumu.
Mhe. Mwanaidi akizungumza na watoto na walezi wa kijiji cha Matumani alipokitembelea leo jijini Dodoma amesema wadau wote wana wajibu wa kuwatunza watoto hao ili kutengeneza Taifa bora la baadaye.
Mwanaidi amekipongeza kituo hicho kwa kuwalea watoto katika mazingira mazuri na kuwa ni mfano wa kuigwa kwa kusaidiana na Serikali kuhakikisha watoto wote wanapata malezi bora.
“Suala la kulea watoto yatima siyo jambo la mtu mmoja au la Serikali pekee. Jamii yote tushirikiane kuwasaidia watoto hawa kwa hali na mali” alisema Mhe. Mwanaidi.
Mtoto Glory Said akisoma risala kwa niaba ya watoto wenzake ameiomba jamii iendelee kuwapatia misaada mbalimbali hususani chakula na mahitaji mengine ili waweze kuishi kwa furaha.
Kwa upande wake Meneja wa kituo hicho Padre Vincent Bozeli ameishukuru Serikali kwa kukitambua kituo hicho kama sehemu ya kusaidia watoto wanaoishi katika mazingira magumu.