Na: Lilian Lundo – MAELEZO, Dodoma.
Serikali imesema inafanya marekebisho ya tozo mbalimbali kwa wafanyabiashara wakiwemo wafanyabiashara wa pembejeo za kilimo ili kuwawezesha wafanyabiashara hao kupata pembejeo na kuzipeleka mpaka ngazi za Vijiji.
Hayo yameelezwa leo Bungeni, Jijini Dodoma na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Madaba, Joseph Mhagama juu ya mpango wa Serikali katika kupunguza tozo za maduka yanayouza pembejeo ili kuwawezesha wakulima kupata pembejeo hizo hata katika ngazi ya Vijiji na kwa gharama nafuu.
“Ni kweli kwamba Serikali imepokea ushauri na malalamiko kadhaa kutoka kwa Wafanyabiashara mbalimbali wakiwemo wafanyabiashara wa maduka ya pembejeo juu ya tozo mbalimbali katika uendeshaji wa shughuli nzima za biashara,” amesema Waziri Mkuu.
Amesema kuwa, kazi kubwa inayofanywa na Serikali sasa ni kufanya mapitio ya tozo zote ambapo mawaziri wenye dhamana ambao wanatozo mbalimbali kwenye wizara zao zinazokwamisha kufanya biashara katika mazingira rahisi wameshakutana ili kuangalia tozo zinazohitaji kupitiwa upya.
“Kwa sasa mkakati wa Serikali unaendelea na niwape matumaini wafanyabiashara wote nchini kwamba Serikali imesikia vilio vyao, na tunafanya mapitio ya tozo hizo na tutakapofikia hatua nzuri tutawajulisha ili kujua ni aina gani ya tozo tunataka tuiondoe au kuibadilisha ili muendelee kufanya biashara zenu kwa mazingira rahisi,’’ amesema Waziri Mkuu.
Aidha, alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tarime, Esther Matiko juu ya askari kutonunuliwa sare kwa muda mrefu hivyo kupelekea kujinunulia sare hizo wao wenyewe.
Waziri Mkuu amesema, Serikali inayowajibu wa kutoa vifaa mbalimbali zikiwemo sare kwa majeshi ili waweze kufanya kazi zao vizuri. Hivyo basi watawasiliana na Waziri mwenye dhamana ili kujua ni kwa nini askari hao wanajinunulia sare na kama ndo sera ndani ya wizara basi marekebisho yafanyike kadri ya mahitaji.