Baadhi ya madiwani wakiwa kwenye baraza maalumu kwa ajili ya kutafuta njia ya kutatua mgomo wa daladala na bajaji
Na Fredy Mgunda Iringa.
Baraza la madiwani manispaa ya Iringa limepitisha utaratibu mpya wa wa vituo vya kupakia abilia na barabara zitakazo kuwa zinatumiwa na bajaji na daladala zote za manispaa ya Iringa kwa lengo la kutatua mgogoro uliokuwepo baina ya daladala na bajaji.
Akitoa maazimio hayo mbele ya baraza maalum la madiwa lililofanyika tarehe 28 mwezi wa nne mstahiki meya wa manispaa ya Iringa Ibrahim Ngwada alisema kuwa baraza limetafuta njia ya kutatua mgogoro huo kwa kuangalia namna bora ya njia na vituo ambavyo vitatumika.
Alisema kuwa bajaji zote za zamani zinazotoka nje ya mkoa wa Iringa hazitapokelewa na kupewa namba ya usajili na bajaji zitakazopolewa na kusajiliwa ni bajaji mpya na zitapangiwa vituo vya pembezoni mwa mji.
Ngwada alisema kuwa stendi ya miomboni itatumiwa na bajaji za Kihesa na Ipogolo huku daladala zote zitatumia standi kuu ya zamani na bajaji zote za ukanda wa kihesa hazitatumia barabara kuu ya Dodoma na badala yake zitapita barabara ya mama siyovelwa.
Aliongeza kwa kusema kuwa bajaji zote za ukanda wa ipogolo zimeruhusiwa kupandisha juu kupitia barabara kuu kwa kukatisha kwa mambo kupitia barabara ya Legezamwendo na shooters na kuishia stendi ya miomboni.
Ngwada alisema kuwa ili kuwahudumia wananchi wa kihodombi itarudisha njia ya daladala ya Kihodombi Tumaini na daladala zote zirudi kwenye njia zao na kuanza kazi kama ilivyokuwa awali pamoja na marekebisho yake katika maeneo hayo.
Aidha meya Ngwada alisema kuwa vituo vya soko kuu na shooters pamoja na MR vilivyokuwa vinatumia kama stendi ya bajaji vimefutwa.
Kwa upande wake mbunge wa jimbo la Iringa mjini Jesca Msambatavangu alisema kuwa maazimio yaliyotolewa leo na baraza maalum la madiwani ndio maamuzi sahihi kwa lengo la kutatua mgogoro uliokuwepo baina ya daladala na bajaji.
Msambavangu aliwaomba madereva na wamiliki wa bajaji na daladala kupokea na kuyafanyia kazi maazimio yote yaliyotolewa na baraza la madiwani kwa kuwa maazimio hayo yamepitishwa kisheria.
Alimalizia kwa kusema kuwa ameyapokea kwa mikono miwili maazimio hayo tofauti na ilivyokuwa hapo awali walipotoa maamuzi bila kujadili kwa kina namna ya kutatua mgogoro na ndio ilikuwa sababu ya kuyapinga maamuzi ya awali yaliyokuwa yametolewa.
Nao viongozi wa bajaji na daladala walisema kuwa wameyapokea maazimio hayo na wanakwenda kuyapitia na kutafakari kwa kina ndio watoe tamko kama wataendelea kufanya kazi au kuendelea na mgomo.