Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba akifungua kikao cha uzinduzi Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweden jijini Dodoma jana.
Balozi wa Sweden nchini Mhe. Anders Sjoberg akiwa katika kikao cha uzinduzi Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweden jijini Dodoma jana.
Mratibu wa Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) Julius Enock akiwasilisha mada kuhusu mradi huo katika kikao cha uzinduzi Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweden jijini Dodoma jana.
Washiriki wa kikao cha uzinduzi Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweden wakiendelea na majadiliano katika kikao hcho jijini Dodoma jana.
***************************************
Serikali kupitia Ofisi ya Makamu wa Rais kwa ushirikiano na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imezindua Mradi wa Kuimarisha Uwezo wa Kitaasisi wa Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (EMA) chini ya ufadhili wa Serikali ya Sweden jijini Dodoma jana.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo Mkurugenzi wa Idara ya Mazingira Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Andrew Komba alisema mradi huo utasaidia kuongeza uwezo wa kitaasisi wa mamlaka husika za udhibiti kwa kuimarisha uzingatiaji wa sheria na mifumo ya utekelezaji.
Dkt. Komba alibainisha kuwa Serikali imefanya jitihada kadhaa za kulinda na kuhifadhi mazingira ikiwa ni pamoja na kuweka Sera ya Kitaifa ya Mazingira (1997), ambayo inaendelea kuboreshwa pamoja na Sheria ya Usimamizi wa Mazingira (2004).
Alisema kuwa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira Sura ya 191 inatoa mfumo wa kiutawala na kitaasisi wa usimamizi wa mazingira nchini ambao unapita katika ngazi zote za utawala wa Serikali.
Akifafanua zaidi alisema EMA inakusudia kuboresha uratibu wa usimamizi wa mazingira nchini unaokusudia kushughulikia changamoto kuu za mazingira na kuondoa vizuizi vya kisekta ambavyo kila Wizara ina mamlaka maalumu ya kisheria na wigo wa utendaji.
“Utekelezaji wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira umekabiliwa na changamoto kadhaa na bado kuna uwezo mdogo uliopo ukiwemo rasilimali watu na miundombinu na rasilimali fedha duni katika utekelezaji, ufuatiliaji na tathmini ya rasilimali mazingira katika ngazi zote. Uwezo katika ngazi ya Serikali za Mitaa umekuwa chini,” alisema.
Kutokana na changamoto hizo Mkurugenzi huyo alibainisha umuhimu wa kuimarisha uwezo katika mkoa na Serikali za Mitaa, kwani hawa wanawajibika zaidi kwa usimamizi wa mazingira.
Aliishukuru Serikali ya Sweden kwa niaba ya Tanzania na kusema dhamira ya Serikali ni kutoa kipaumbele katika kuhakikisha kuwa mradi huo unatimiza malengo yake.