……………………………………………………………………….
Naibu Waziri Ofisi ya Rais-Utumishi, Deo Ndejembi amesema kuwa Serikali imeahidi kuwapandisha madaraja watumishi wa umma takribani 90,000 lengo likiwa ni kuonesha namna wanavyowajali huku akiwataka pia kutimiza wajibu wao.
Naibu Waziri Ndejembi ametoa kauli hiyo alipokua akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambapo pia amewaonya watumishi hao kuacha kufanya kazi kwa mazoea na badala yake watimize wajibu wao kwa kuzingatia weledi, sheria na maadili ya kazi zao.
Ndejembi amesema serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ipo tayari kushirikiana na watumishi wote nchini na ndio maana kupitia wizara hiyo ya Utumishi wametangaza kupandisha madaraja hayo akifahamu fika kuwa ni kilio cha muda mrefu.
” Siyo mnachekelea kuona sisi serikali tunawapandishia madaraja ilihali nyie utendaji wenu wa kazi, Ofisi ya Rais-Utumishi haitomvumilia mtumishi yeyote ambaye ataleta uzembe kazini haitomvumilia Afisa Utumishi yeyote atakayekua akiwaonea watumishi wa umma.
Wapo watumishi wasio waadilifu hawa niwahakikishie sisi hatutowaacha tutaruka nao, mfano hapa Chamwino nafahamu kuna Afisa Ardhi, anaitwa Charles Laseko ambaye ameuza eneo la Wananchi wa hapa kimakosa tena bila kuzingatia sheria za kazi nikuagize Mkurugenzi wa Halmashauri kumuandikia barua kali ya onyo na nakala niipate, yoyote ambaye ataenda kinyume tutamshughulikia,” Amesema Ndejembi.
Amewataka maafisa utumishi wote nchini kuacha kujifanya miungu watu na wanapaswa kujua ni kazi yao kutoa huduma kwa watumishi wanaotoa huduma kwa watanzania, ambaye ataenda kinyume hatutomvumilia.
” Nisisitize tubadilike, haya malalamiko yanayotolewa kwa Maafisa Utumishi kuwa hawapeleki kwa wakati changamoto za watumishi wao kwenye mamlaka husika, hawatumi majina ya watumishi wanaopaswa kupandishwa Daraja, hii changamoto tumeiona Nchi nzima nirudie tena hatutovumilia wale wote wanaojiona miungu watu,” Amesema Ndejembi.