Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe.Ummy Mwalimu,akizungumza na watendaji wa ngazi za juu za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma leo April 14,2021.
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge,akisisitiza jambo kwa watendaji wa ngazi za juu za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma,kulia ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe.Ummy Mwalimu.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Vumilia Nyamoga,akizungumza wakati wa watendaji wa ngazi za juu za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma leo April 14,2021.
Baadhi ya watumishi wakimsikiliza Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe.Ummy Mwalimu,alipokuwa akizungumza na watendaji wa ngazi za juu za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma leo April 14,2021.
……………………………………………………………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Serikali imewaagiza watendaji wa Halmashauri zote hapa nchini kuacha tabia ya kuwadharau na kupuuzia ushauri wa madiwani wanapowashauri katika mambo ya kiutendaji kwenye maeneo yao ya kazi kwani wao ndio wanajua mambo mengi kwa kuwa ndio wawakilishi wa wananchi.
Maagizo hayo yametolewa Wilayani Chamwino na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Ummy Mwalimu wakati akizungumza na watendaji wa ngazi za juu za watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma.
Amesema kuna baadhi ya watendaji wanapuuzia na udharau na kutotendea kazi ushauri wa wanasiasa wanapowashauri katika mambo mbalimbali hasa yanayohusu vyanzo vya mapato katika halmashauri hizo.
“Nitoe wito kwa Halmashauri zote hapa nchini kuacha mara moja hii tabia ya kuwadharau wanasiasa, kwa kudhani madiwani wote ni darasa la saba, hapana, sasa hivi kuna madiwani wana PHD, n a hata kama darasa la saba hao wamechaguliwa na wananchi na wanajua mambo mengi sana yanayohusu wananchi” amesema Waziri Ummy.
Amewataka watendaji wa Halmashauri zote hapa nchini kufanya kazi kwa kushirikiana na kushirikishana katika kutimiza majukumu yao huku wakishirikiana wakaweke mkazo katika ukusanyaji wa mapato ya serikali na kuyaingiza katika mfumo bila kuyafuja.
Waziri Ummy pia amemuagiza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ndani ya siku tatu kuhakikisha mapato yote yaliyoainishwa na Mkaguzi na mdhibiti wa hesabu za Serikali CAG kuwa yalikusanywa na hayajaingizwa benki ndani ya siku tatu mapato yote yawe yameingizwa benki.
Aidha Waziri ummy amesema hata mvumilia Mkurugenzi wa Halmashauri yoyote ambaye hata tenga asilimia 40 ya fedha anazozikusanya na kuzielekeza katika shughuli za maendeleo na kuzitaka halmashauri kuweka kipaumbele katika miradi ya afya katika maeneo yao.
Aidha amezikumbusha sekretarieti za Mikoa kuhakikisha zinatimiza majukumu yao katika kuzishauri halmashauri hasa katika ukusanyaji na matumizi ya mapato katika serikali za mitaa na kujenga utamaduni wa kuzitembelea na kufanya tathmini katika yale waliyoyapanga.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt Binilith Mahenge amesema kwa kipindi kirefu halmasahuri ya Wilaya ya Chamwino imekuwa haifanyi vizuri licha ya juhudi nyingi ambazo wamezifanya katika kuhakikisha inaimarika katika kipengele cha kukusanya na katika matumizi sahihi ya mapato ya Serikali.
Amesema Wilaya ya Chamwino kijiografia ni kubwa ukilinganisha na Wilaya nyingine lakini bado imekuwa ikifanya vibaya katika ukusanyaji wa mapato ya serikali katika Wilaya hiyo.