Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Babati.
………………………………………………………………………………………..
Na Mwandishi wetu, Babati
TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU Mkoani Manyara, inamshikilia karani wa Mahakama ya mwanzo Magugu Wilayani Babati, Alfred Jackson Ntatirwa kwa kudaiwa kuomba na kupokea rushwa ya shilingi elfu 30 ili ampatie mwananchi nakala ya hukumu.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Babati, Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amesema tukio hilo limetokea Aprili 6 mwaka huu mji mdogo wa Magugu.
Makungu ameeleza kuwa Ntatirwa anadaiwa kufanya makosa hayo kinyume na kufungua cha 15 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.
Amesema karani huyo Ntatirwa anatuhumiwa kuomba rushwa ya shilingi elfu 30 na kukamatwa na maofisa wa TAKUKURU akiwa amepokea kiasi hicho cha fedha ili atoe nakala ya hukumu ya kesi.
Amesema Ntatirwa aliomba fedha hiyo ili amsaidie mtu mmoja aliyeomba nakala ya hukumu ya kesi iliyokuwepo mahakama ya mwanzo Magugu ambaye hakuridhika na hukumu hiyo na alitaka kukata rufaa mahakama ya Wilaya.
Ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo anatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote ili akajibu mashtaka hayo yanayomkabili.
“Wananchi wote wanapaswa kufahamu kuwa hawalazimiki kulipia tozo yoyote inayohusiana na nakala za hukumu na maamuzi ya mahakama Kuu, mahakama ya Hakimu mkazi na mahakama ya mwanzo,” amesema Makungu.
Amesema Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma alikwashatoa maelekezo kwa mahakama zote nchini kuwa hawatalazimika kulipa tozo yoyote kuhusiana na nakala za hukumu na maamuzi mbalimbali kwa maana ya Judgement, Rulings, Order, Decrees and Drawn orders.
“Kwa hiyo mwananchi yeyote akidaiwa fedha katika orodha hiyo fahamu kuwa ni rushwa na unapaswa kutoa taarifa TAKUKURU kwa kutumia namba za dharura 111 ili hatua stahiki zichukuliwe,” amesema Makungu.