……………………………………………………………………………..
Na Alex Sonna, Dodoma
Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa OR TAMISEMI anayeshughulikia elimu Mhe. David Silinde amewaonya wakuu wa shule za Sekondari na vituo vya elimu wenye tabia ya kuwadharau maafisa elimu wa kata katika maeneo yao.
Pia amewaonya maafisa elimu wenye tabia ya kujikita katika shule za msingi pekee na kushindwa kutembelea shule za sekondari katika kutekeleza majukumu yao.
Naibu Waziri Silinde ameyabainisha hayo Jijini Dodoma wakati akifungua mkutano maalumu wa wawakilishi wa umoja wa maafisa elimu wa kata hapa nchini UMEKTA, ambapo amesema kumekuwa na tabia ya baadhi ya shule za Sekondari kuwadharau maafisa elimu wa kata zao wanapotimiza majukumu yao.
“Kumekuwa na tabia baadhi ya shule za Sekondari hasa zile kongwe na vituo vya elimu wamekuwa wakiwadharau maafisa elimu na hawataki kufanya kazi nao, nawakumbusha maafisa elimu kata ndio wasimamizi wa shughuli zote za elimu kwenye kata,
Pia kuna tabia ya maafisa elimu kujikita kusimamia shule za msingi pekee sijui wanaogopa nini au wanadhani huko ndio kunakohitajika usimamizi hapana kote kusimamiwe” amesema Mhe. Silinde.
Amebainisha kuwa katika awamu hii kutokana na kutoa elimu bure kwa shule za msingi na sekondari kwa kidato cha kwanza hadi cha nne kumeleta mafanikio makubwa kutokana na kuongezeka kwa wanafunzi wanaoandikishwa kuanza elimu ya awali, msingi na sekondari.
Pia kuongezeka kwa ufaulu kwa shule za msingi na sekondari, kuboreka kwa ufundishaji wa wanafunzi wenye mahitaji maalum, uandikishaji elimu maalum, awali, msingi na sekondari umeongezeka amewataka maafisa elimu kwenda kusimamia kikamilifu ufundishaji wa walimu katika shule hizo.
“Bado kunachangamoto kwenye maeneo mnayosimamia kwani kuna wanafunzi wasioweza kumudu kusoma kuandika na kuhesabu kuanzia darasa la kwanza hadi la nne,
baadhi ya maeneo mwalimu baada ya kumaliza kipindi anakwenda kulewa, hadi usiku wa manane akiamka anakwenda kufundisha akiwa ananuka pombe wanawafunza nini wanafunzi” amesema.
Aidha Mhe. Silinde amewaagiza maafisa elimu kata kwenda kusimamia miradi yote ya maendeleo inayopelekwa na serikali iwe wizara ya elimu au TAMISEMI ikiwemo kusimamia kwa kikamilifu miradi, raslimali watu katika maeneo yao na fedha zote za miradi zinazokwenda kwenye maeneo yao.
“Kama mnanyimwa taarifa mtupatie TAMISEMI tutachukua hatua, wengine tunawaweza nawang’oa huko huko, serikali imepeleka fedha nyingi sana lakini kuna shida ya kufichana taarifa kwenye maeneo yenu,” amesema.
Amewataka maafisa elimu kila mmoja kuhakikisha taarifa zinazoingizwa kwenye mfumo zinakuwa ni sahihi, na watakaoshindwa kufanya hivyo watawachukulia hatua kwa kuidanganya serikali kwani baadhi ya maeneo taarifa zinakinzana na taarifa za NECTA.
Pia amewataka maafisa elimu kwenda kutoa elimu ya madhara ya mikopo kwa walimu kwani baadhi wamekuwa na mikopo mingi kupita kiasi na kukosa utulivu kwenye suala zima la ufundishaji.
Awali, Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI anayeshughulikia elimu Gerald Mweli, amesema maafisa elimu kata awali walikuwa wakiitwa waratibu wa elimu Kata lakini sasa wamebadilishiwa jina nakuitwa maafisa elimu sambamba kuongeza vigezo na lazima awe na elimu ya shahada (Digree).
Pia ameagiza maafisa elimu Mikoa na Wilaya kwenda kuwajengea uwezo maafisa elimu kata ili kuelewa majukumu yao vyema katika kata zao katika kuboresha elimu hapa nchini na kubainisha kuwa kundi hilo limegaiwa pikipiki nchini nzima katika kuboresha utendaji kazi wao.
Nae mwenyekiti wa umoja huo bw. Robart Tesha amesema mkutano huo ni wa siku mbili wenye lengo la kupitia katiba ya umoja huo kabla ya kwenda kuisajili rasmi ili iweze kutambulika na mamlaka husika.
Amesema mkutano huo umeshirikisha viongozi wawili wa umoja huo kutoka kila Halmashauri ambapo inafanya kufikia idadi ya 368 ambapo maada mbalimbali kutoka kwa viongozi wa taasisi mbalimbali zitawasilishwa.