Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) akikata utepe kuashiria Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini katika Warsha ya Uzinduzi wa Mpango huo inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah ( wa nne kutoka kulia) akionesha wadau Kitabu cha Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini muda mfupi baada ya kukizindua katika Warsha inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30- 31, 2021. Wa pili kutoka kulia ni Mwenyekiti wa Kikosi Kazi cha Taifa cha Kuandaa Mpango Kazi wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini, Yahya Mgawe.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akiongea na wadau wa uvuvi (hawapo pichani) wakati akifungua Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini ambapo alieleza kuwa Uvuvi mdogo una mchango mkubwa katika kuhakikisha usalama wa chakula na kuondoa umasikini hasa katika nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania.Warsha hiyo ya siku mbili inafanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah akiongea na Wadau wa Uvuvi (hawapo pichani) wakati akifungua rasmi Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Sehemu ya Wadau wa Uvuvi waliohudhuria Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini wakifuatilia matukio yanayoendelea katika Warsha hiyo inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Mkurugenzi wa Uvuvi, Emmanuel Bulayi (kushoto) akimkaribisha Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah (kulia) ili afungue rasmi Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kitaifa wa kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini unaofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
…………………………………………………………………………………………
Na Mbaraka Kambona,
Katibu Mkuu, Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Uvuvi), Dkt. Rashid Tamatamah amesema kuwa utashi wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati, Dkt. John Magufuli wa kuamua kuwekeza katika Sekta ya Uvuvi umechangia kwa kiasi kikubwa maendeleo ya sekta hiyo.
Dkt. Tamatamah alisema hayo alipokuwa akifungua Warsha ya Uzinduzi wa Mpango Kazi wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo nchini inayofanyika Mkoani Morogoro kuanzia Machi 30-31, 2021.
Akiongea na wadau wa Sekta ya uvuvi waliohudhuria warsha hiyo ya siku mbili, Dkt. Tamatamah alisema kuwa utayari wa Hayati Dkt. Magufuli kuwekeza katika sekta ya uvuvi umesababisha kuanzishwa kwa miradi mbalimbali ya maendeleo katika sekta hiyo.
“Sisi ambao tupo katika ngazi za juu za Wizara tunatambua kwamba utayari wake wa kuona kwamba mchango wa sekta ya uvuvi unakuwa mkubwa katika pato la Taifa umepelekea mipango mikubwa ya uwekezaji ambayo itatekelezwa wizarani katika mwaka ujao wa fedha,” alisema Dkt. Tamatamah
Aliendelea kusema kuwa utayari wake wa kununua Meli nane (8) za kufanya uvuvi katika bahari kuu ulipelekea timu ya wataalamu wa Serikali iliyokuwa kwenye majadiliano na Shirika la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD) kuhusu mkopo wa kuendeleza sekta ya uvuvi waweke kipaumbele ununuzi wa meli hizo miongoni mwa vitu vitakavyofadhiliwa na mradi huo.
“Katika mwaka ujao wa fedha 2021/22, Serikali itatumia kiasi cha shilingi Bilioni 50 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Bandari ya kwanza ya uvuvi ambao utafanyika katika eneo la Mbegani Bagamoyo, hizi zote ni juhudi na msukumo wake,”alifafanua Dkt. Tamatamah
Aidha, Dkt. Tamatamah alisema pamoja na nchi kupata msiba huo, uongozi uliopo sasa chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan hakuna shaka kuwa mipango yote ya uwekezaji iliyoachwa na Hayati, Dkt. Magufuli katika Sekta ya Uvuvi itatekelezwa kama ilivyopangwa ili kutimiza malengo yaliyowekwa katika utawala wake.
Kuhusu Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutekeleza Mwongozo wa Hiari wa Uendelezaji wa Uvuvi Mdogo Nchini, Dkt. Tamatamah alisema kuzinduliwa kwa mpango huo kutakuwa ni ukombozi kwa wavuvi wadogo kwa sababu mwongozo huo umeweza kuonesha njia bora zitakazowezesha hali ya wavuvi wadogo kuimarika na kuinua uchumi wao.
“Mpango huu utasaidia wavuvi wadogo kufanya uvuvi endelevu ikiwemo kusimamia rasilimali za uvuvi katika muktadha wa chakula na kuondoa umasikini,” alisema Dkt. Tamatamah
Kwa upande wa wadau, Katibu wa Kikundi cha Ulinzi Shirikishi cha Rasilimali za Bahari (BMU), Kilindoni, Wilayani Mafia alisema kuwa wanaishukuru serikali kutambua mchango wa wavuvi wadogo na kuamua kuandaa mpango huo ambao utawasaidia kupata masoko ya uhakika na zana bora za uvuvi kwa ajili ya uvuvi endelevu.
Naye, Suzana Ezekiel, Mvuvi Mdogo anayefanya shughuli zake katika Mwalo wa Kibirizi, Kigoma alisema kuwa wavuvi wengi wadogo bado wanafanya shughuli zao kwa kubahatisha lakini Mpango kazi huo utawawezesha kuondokana na hali hiyo na kufanya uvuvi endelevu na wa uhakika.