Baadhi ya waombolezaji wakiwa kwenye uwanja wa CCM Vwawa ambako jeneza la mwili wa marehemu William Mwamlima uliwekwa kwaajili ya kuagwa na wananchi wa mji wa Vwawa na vitongoji vyake
Mwenyekiti wa chama cha Mpira wa miguu mkoani Mbeya na Mjumbe wa kamati ya Utendaji ya TFF Elias Mwanjala akitoa heshima za mwisho mbele ya mwili wa William Mwamlima leo mchana katika uwanja wa CCM Vwawa wilayani Mbozi
Pichani William Mwamlima enzi za uhai wake.
…………………………………………………
Na Danny Tweve
Mwili wa Mjumbe wa Mkutano mkuu wa Taifa wa TFF ambaye pia alikuwa Katibu wa Chama cha Soka Mkoa wa Songwe Wiliam Mwamlima ameagwa leo kwenye uwanja wa mpira wa CCM Vwawa kuelekea kijiji kwao Iyula kwaajili ya Mazishi mchana wa leo
Mwamlima ambaye amefariki jana saa 2.30 asubuhi nyumbani kwake Vwawa alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa shinikizo la Damu.
Wakitoa salamu za rambirambi za TFF wawakilishi wake Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya Elias Mwanjala na Shafii Dauda wamesema soka la Tanzania limempoteza mtu mhimu kutokana na utayari wake wakati wote kushughulia masuala ya soka ya Mkoa na Taifa.
Mwamlima alianza kupata shinikizo la damu akiwa kwenye mashindano ya vijana wa chini ya umri wa miaka 17 yaliyofanyika mwezi Juni jijini Dar es salaam akiongoza timu ya Mkoa wa Songwe, na tokea kipindi hicho hali yake iliendelea kuwa dhaifu.
Mwamlima alikuwa mwenyekiti wa chama cha soka wilaya ya Mbozi kati ya mwaka 1999 hadi 2007, alihudhulia mafunzo ya ualimu wa mpira ngazi ya intermediate kati ya 2009-2010, alichakuliwa kuwa katibu wa MBOFA (2008-2014 na Katibu msaidizi wa Chama cha Soka Mkoa wa Mbeya kati ya 2014 hadi 2015.
Mwaka 2016 hadi kifo chake alikuwa Katibu wa Chama cha Soka mkoa wa Songwe-SOREFA na pia mjumbe wa Mkutano mkuu wa Taifa TFF.
Shirikisho la Mpira TFF limetoa ubani wa Tshs 500,000 kwa msiba huo huku viongozi wengine wa mkoa akiwemo Mkuu wa mkoa wa Songwe Brigedia Jenerali Mwangela wametoa 100,000/=, Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Mbozi Elick Ambakisye 100,000/= na wadau wengine wa soka wameendelea kutoa michango ya rambirambi kwa familia ya Mwamlima.
Wiliam Mwamlima alizaliwa mwaka 10/8/1968 katika kijiji cha Iyula wilayani Mbozi.