Na Dotto Mwaibale, Singida.
MTENDAJI Mkuu Taasisi ya Uboreshaji Maadili kwenye Utumishi wa Umma na Sekta Binafsi Tanzania (WoLaOTa), Samwel Olesaitabau ametuma salamu za rambirambi kufuatia kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati John Pombe Joseph Magufuli kilichotokea siku ya Jumatano majira ya saa 12:00 jioni Machi, 17/2021, katika Hospitali Nzela Dar es Salaam.
Akitoa salamu hizo mbele ya wanahabari mjini hapa, Olesaitabau alisema kuwa ni tukio lililoshtua wengi maeneo mbalimbali ya nchi, ni tukio lililoshtua watu wengi wa Afrika Mashariki na Maziwa Makuu, ni tukio lililokuja wakati ambapo watanzania wengi walianza kuwa na imani ya utawala wake, ni tukio ambalo hata baadhi ya nchi rafiki duniani limewashtua sana, ni tukio ambalo limewaacha watu wengi kutoamini masikio yao.
Ni tukio lililobeba huzuni kubwa kwa watanzania walio wengi, ni tukio lililokatisha ndoto njema kwa nchi yetu na ni tukio ambalo litaendelea kugonga vichwa vya watanzania kwa kipindi kirefu.
Alisema kwa niaba ya taasisi anatoa pole kwa Mwalimu Janeth Magufuli na familia yake kwa kuondokewa na mwenzi wake.
“Nimpe pole Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuondokewa na Rais wake wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli,
nimpe pole mama yetu Samia Suluhu Hassani kwa kuondokewa na mtu muhimu aliyekuwa mbele yake katika kuongoza nchi, nitoe pole sana kwa Waziri Mkuu na Baraza zima la Mawaziri kwa msiba huu Mkubwa,” alisema Olesaitabau.
Olesaitabau ametoa pole kwa viongozi wa Serikali kuanzia ngazi ya Shina hadi Taifa kwa msiba huu mkubwa, nitoe pole nyingi kwa wanachama wote wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuondokewa na Mwenyekiti wao ndugu John Pombe Magufuli na kuwa jambo lililo kubwa sana watanzania waamini hili limetokea na hakuna jinsi zaidi ya sisi kuendeleza upendo kama alivyoanzisha Hayati John Magufuli.
Alisema watanzania tunapaswa kuamini kwamba, hii ni mipango ya Mungu, tumuombee ndugu yetu Magufuli ili awe mahali salama huko ahera huku tukijipa moyo mkuu na kuamini Mungu anajua atakapo tupeleka baada ya tukio hili.
“Tuendelee kumtukuza yeye John Magufuli kwa kutenda yale aliyoyataka yawe kabla ya umauti kumkuta.Tuombe sana Mungu atupe mbadala sahihi wa Hayati Magufuli.
Niwaombe watanzania kuacha kuhesabu mabaya ya ndugu yetu Magufuli, niwaombe watanzania wajue kwamba, hakuna binadamu aliyekamilika na wajue kwamba,ili mwanadamu akamilike lazima awe na dhaifu zake, niwaombe wayazungumzie yale mazuri mengi aliyotenda mpendwa wetu Magufuli,” alisema Olesaitabau.
Olesaitabau aliwaomba watanzania wayakabidhi yale madhaifu ya ndugu yetu hayati Magufuli kwa Mungu na kuyanena mazuri yake kila wakati ili roho yake ikae mahali salama huko Mbinguni na kuwa wakubali kwamba, mipango ya maisha yetu yapo kwa Mungu na hivyo tusimtafute mchawi bali tumuombee John Joseph Magufuli apokelewe kwenye ufalme wa Mbingu.
YATAKAYOKUMBUKWA NA WATANZANIA KUHUSU HAYATI MAGUFULI;
Olesaitabau alisema japo hawezi kuwasemea watu wengine lakini wao kama Taasisi inayo jali maadili mema kwenye utendaji wa kila siku kwa watendaji wa Serikali na Watumishi wa Umma wataendelea kumkumbuka Hayati John Magufuli kwa mengi na baadhi ya mambo hayo ameyataja kuwa ni kama rais aliyekuwa na msimamo thabiti wa kusimamia kile anachoamini kwamba ni sahihi, kuamini kwamba Bara la Afrika linaweza kujitegemea kwa kutumia rasimali zao wenyewe, atakumbukwa kwa alama nyingi alizoacha kupitia utendaji wake, mfano.Barabara za juu, reli na hata bwawa kubwa la umeme la Rufiji na kadhalika.
Aidha, Olesaitabau alisema Magufuli atakumbukwa na watanzania maskini kwa kujitolea kwa nguvu zote kupambana na wabadhirifu wa mali ya umma, kuanzisha mfumo wa ukusanyaji KODI uliyoziba, kama sio kupunguza mianya ya Rushwa na Ufisadi, atakumbukwa kwa kuanzisha mfumo wa udhibiti wa rasilimali fedha zinazopelekwa kwenye halmashauri kwa ajili ya maendeleo.
Olesaitabau ataja mambo mengine ambayo atakumbukwa ni kurudisha maadili mema katika Utumishi wa Umma na yeye mwenyewe kuwa mfano, kuthubutu na kufanikiwa kuleta Elimu Msingi Bure, kuwa Rais aliyependa kila Kiongozi kuwajibika kwa nafasi yake, Rais asiyeyumbishwa kwa haraka na kelele kuhusu alichodhamiria, Rais ambaye hayupo tayari kulalamika pale anapokutana na changamoto, atakumbukwa kama Rais ambaye alikuwa na sauti ya kiutawala na kuwafanya walio chini yake kutekeleza yale yaliyo ya faida kwa watanzania wanyonge. Atakumbukwa kama Rais ambaye hapendi mtu wa chini kuonewa.Atakumbukwa kama Rais ambaye hakupenda wateule wake kutoa majibu ya ubabaishaji.
Alitaja mambo mengine atakayokumbukwa ni kiongozi aliyekuwa na kipaji cha kuhifadhi kumbukumbu kichwani, ni kiongozi aliyetoa nafasi ya kujirekebisha pale inapobidi kwa wateule wake kabla ya kuwaondoa kwenye nafasi zao, atakumbukwa kama kiongozi aliyejua kwamba, uongozi ni gharama na unahitaji kujitoa Muhanga, atakumbukwa kama Rais aliyeonyesha kwa vitendo maana ya uadilifu, atakumbukwa kwakutaka kufuata nyayo za Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere hasa katika suala la kujitegemea kamaTaifa, Magufuli atakumbukwa kama mtu aliyeamini kwamba,uongozi ni utumishi wa Mungu kama ilivyoandikwa na mtumishi wa Mungu Mathayo kupitia Sura 20:26-28 na maneno ya Mungu yanasema; ”Lakini kwenu isiwe hivyo ila anayetaka kuwa mkuu kati yenu sharti awe mtumishi wa wote, na anaye taka kuwa wa kwanza kati yenu sharti awe mtumishi wenu ,na hivyo hivyo mwana wa Mungu hakuja kutumikiwa bali amekuja kutumika na kutoa maisha yake kuwa fidia ya watu.”
Olesaitabau alisema Magufuli atakumbukwa kama kiongozi aliyekuwa na uwezo wa ubunifu kama alivyosema Mwanafalsafa mmoja wa uongozi aitwaye Steve Jobs miaka ya hivi karibu ninanaomba ninukuu;”Ubunifu ndiyo hutofautisha kiongozi na wafuasi wake,na kwavyovyote vile ukitaka kusonga mbele katika Ulimwengu wa sasa lazima uwe na kiongozi mbunifu” kama alivyokuwa Hayati Magufuli.
WITO
Olesaitabau ametoa wito kwa Watanzania tuendelee kushikamana zaidi na tuachanena yale yote yatakayo tugawa sisi kamaTaifa, niwaombe waliyopo kwenye Serikali hivi sasa waendelee kuchapakazi na kamwe wasilegeze kamba na kwa kufanya hivyo watanzania wataendelea kuwa mahali salama hata baada ya kifo cha Hayati John Pombe Magufuli.
“Nimuombe Rais Mama Samia na Serikali yake asiache kusimamia yale mazuri yote aliyoanzisha mpendwa wetu hayati John Magufuli, kuendelea kusimamia ule mfumo wa ukusanyaji KODI kwa faida ya Watanzania, kuendelea kuziba ile mianya ya wizi wa mali ya Umma kama alivyofanya hayati Magufuli na kwa kufanyahivyo, atakuwa amemuenzi,” alisema.
Katika hatua nyingine Olesaitabau amewaomba watanzania kumpa ushirikiano wa kutosha Mama Samia ili kazi yake ya kuongoza nchi iwe rahisi kwake . Na alihitimisha kutoa salamu hizo za rambirambi kwa kufuata maandiko matakatifu kutoka katika kitabu cha AYUBU; 1:21. Na maneno ya Mungu yanasema,” Bwana Ametoa na Bwana Ametwaa jina lake LIHIMIDIWE MILELE”.