BARAZA Kuu Waislamu Tanzania (BAKWATA), Mkoa wa Mwanza, limepokea kwa masikitiko makubwa taarifa ya kifo cha Rais John Magufuli na kuwaasa Watanzania kushikamana,kuwa wavumilivu katika kipindi hiki kigumu cha kuondokewa na kiongozi wao mpendwa.
Rais Magufuli alifariki jana katika Hospitali ya Mzena kwa matatizo ya maradhi ya mfumo wa umeme wa moyo ambapo kabla ya kufikwa na mauti alilazwa Machi 6,mwaka huu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
Akizungumza na waandishi wa habari jana ofisini kwake,Sheikh wa Mkoa wa Mwanza,Alhaji Hasani Kabeke,alisema Watanzania katika kipindi hiki kigumu cha majonzi cha kuondokewa na kiongozi mkuu wa nchi,Rais Magufuli,hivyo washikamane na kuwa watulivu na wavumilivu.
Sheikh Kabeke alisema akiwa kiongozi wa dini na Mwenyekiti Mwenza wa Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Mwanza,amepokea kwa masikitiko na huzuni kubwa kifo cha Rais Magufuli.
Alisema kwa hiari yake Mwenyezi Mungu ndiye aliyemuumba Rais John Magufuli na ndiye aliyemfanya atokee ulimwenguni,yote aliyofanya,karama alizokuwa nazo na utukufu,yote aliyofanya alipewa na mola wake kama zawadi naye hakuwa na hiana aliwatumikia zawadi hiyo kwa kuwatumikia Watanzania kwa unyenyekevu na kwa moyo wote hadi umauti unamkuta.
“Leo tarehe 18, 2021 tumepambazukiwa na siku ya huzuni katika taifa letu la Tanzania,Watanzania wameamka wakiwa na taarifa kutoka kwa Makamu wa Rais,Mama Samia Suluhu Hassani,akieleza jana usiku kwamba mpendwa wetu,kipenzi chetu,jemedari na kiongozi wetu, Rais John Joseph Magufuli, amefariki dunia,”
“Nikiwa Sheikhe wa Mkoa wa Mwanza,kwa hakika tumepokea kwa huzuni kubwa msiba huu mzito,kwa niaba ya Baraza Kuu la Waislamu (BAKWATA, kwa niaba ya Waislamu wa Mkoa wetu na taasisi zote za Kiislamu sababu BAKWATA ndio mwamvuli wa Waislamu,nawajibika kutoa pole za dhati kwa familia ya Rais John Magufuli,mkewe Mama Janeth,watoto,wazazi,ndugu na jamaa kwa kuondokewa na kiongozi wa familia,”alisema Sheikhe Kabeke.
Alisema kwa hakika kiongozi huyo aliyetangulia mbele ya haki mema yake hayafichiki,hivyo Watanzania watamkumbuka sana kwa mambo mengi lakini moja kubwa ni utamaduni wake na tabia ya kumtanguliza Mwenyezi Mungu mbele kwenye kila jambo.
Kuhusu ufanisi wa kazi tangu akiwa Waziri wa Ujenzi,Marehemu Rais Magufuli,katika kutekeleza majukumu yake sote ni mashahidi miradi mikubwa ya maendeleo ametuachia katika taifa letu na kama ambavyo alimweka Mungu mbele kwa kila jambo ambapo katika moja ya hotuba zake aliwahi kusema jambo likiwa gumu kwako hilo mwachie Mungu,hakuna Mtanzania asiyeamini kifo na kikija hakichagui wala hakicheleweshwi.