Home Mchanganyiko MASHAMBA DARASA YA UFUGAJI SAMAKI KUANZISHWA KOTE NCHINI

MASHAMBA DARASA YA UFUGAJI SAMAKI KUANZISHWA KOTE NCHINI

0

Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji ikishuhudia moja ya mabwawa ya kufugia samaki wazazi aina ya sato mara baada ya kutembelea kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, wakiongozwa na mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Dkt. Christine Ishengoma ambapo wameridhishwa na namna kituo hicho kinavyofuga samaki hao na kutaka uwepo wa samaki wazazi ambao watatoa vifaranga bora vya samaki. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki (wa kwanza kushoto), akifuatiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma wakati walipokuwa wakipatiwa maelezo na mmoja wa wataalamu (hayupo pichani) juu ya uzalishaji wa vifaranga vya samaki aina ya sato, wakati kamati hiyo ilipotembelea kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

  Muonekano wa sehemu ya vifaranga vya samaki aina ya sato vinavyozalishwa na kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, ambavyo vimekuwa vikisambazwa kwa wateja katika maeneo mbalimbali nchini. Kifaranga kimoja cha samaki aina ya sato kinauzwa Shilingi 100. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma (wa kwanza kulia) akipatiwa maelezo ya mafanikio na mikakati ya uzalishaji wa vifaranga bora vya samaki na Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Imani Kapinga wakati kamati hiyo ilipotembelea kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

Mmoja wa wafanyakazi wa kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro akiwaonesha wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji samaki aina ya kambale ambapo kituo hicho kipo katika mikakati ya kuanza kuzalisha vifaranga vya samaki hao ili kuongeza upatikanaji wake. (Picha na Edward Kondela, Afisa Habari – Wizara ya Mifugo na Uvuvi).

*****************************************

Na. Edward Kondela

Serikali imesema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2021/22 ina mpango wa kuanzisha vituo vya ukuzaji viumbe maji katika halmashauri 80 za wilaya ikiwa na lengo la kuhakikisha kila halmashauri inakuwa na kituo hicho ambacho kitatumika kama shamba darasa kwa ajili ya kufundisha wananchi namna ya kufuga samaki.

Akizungumza jana (17.03.2021) wakati Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji ilipotembelea kituo cha ukuzaji viumbe maji kinachozalisha vifaranga vya samaki cha Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Mashimba Ndaki amesema mkakati wa serikali kupitia vituo hivyo vitakavyokuwepo katika halshamauri zote za wilaya ni kuwa na samaki wengi wafugwao kwa njia mbalimbali ikiwemo ya mabwawa na kufikia uzalishaji wa samaki wa asilimia 50 kwa njia ya kufuga na asilimia 50 wanaotokana na maji ya asili.

“Kupitia tasnia hii ya ukuzaji viumbe maji tunataka kuweka nguvu kubwa ili tuweze kuvuna rasilimali ya uvuvi iweze kusaidia lishe, ajira na kuondoa umasikini kwa wananchi, hivyo wizara inaweka mikakati ya kuhakikisha inafikia malengo yake kupitia tasnia hii.” Amesema Mhe. Ndaki

Aidha, Waziri Ndaki amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi ina mpango wa kuhakikisha inavipa uwezo mkubwa na kuvikarabati vituo vyote vya ukuzaji viumbe maji vilivyopo nchini ili viweze kwenda sawa na uzalishaji wa vifaranga vya samaki kulingana na mahitaji yake.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu wa Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji Mhe. Dkt. Christine Ishengoma ameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuweka jitihada mbalimbali za kuhakikisha inazalisha kwa wingi vifaranga vya samaki pamoja na kutoa elimu juu ya ufugaji wa samaki.

Amesema kamati hiyo itaangalia vyema bajeti ya wizara itakayowasilishwa kwa ajili ya mwaka wa fedha 2021/22 ili iweze kuwa na tija na kuleta matokeo chanya hususan katika tasnia ya ufugaji samaki kwa kuwa bado ni eneo jipya ambalo watu wengi wanahitaji kujifunza na kujiingiza katika ufugaji huo.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ukuzaji Viumbe Maji kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Imani Kapinga amesema kituo cha ukuzaji viumbe maji Kingolwira kilichopo Mkoani Morogoro, katika kutekeleza majukumu yake kati ya mwaka 2010 hadi 2020 kimetoa mafunzo kwa wananchi 11,280 kutoka mikoa mbalimbali pamoja na kuzalisha vifaranga vya samaki aina ya sato zaidi ya milioni sita vilivyosambazwa maeneo mbalimbali nchini.

Katika ziara hiyo, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge, Kilimo, Mifugo na Maji wameipongeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kuhakikisha inakiboresha kituo cha Kingolwira kwa kufanya upanuzi wa baadhi ya majengo kwa ajili ya ukuzaji viumbe maji na kuiomba wizara izidi kufanya maboresho zaidi katika maeneo ambayo yanahitaji kufanyiwa kazi kufuatia ushauri mbalimbali uliotolewa na wajumbe hao.