Ni Askofu wa kanisa la kiinjili la kirutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Askofu Dkt.Solomon Massangwa
************************************
NA NAMNYAK KIVUYO, ARUSHA.
Askofu wa kanisa la kiinjili la kirutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati Askofu Dkt.Solomon Massangwa amewataka watanzania kupokea kifo cha aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dkt.John Magufuli pamoja na kuiombea nchi kuendelea kuwa na amani na utulivu katika kipindi hiki kigumu.
Askofu Dkt Massangwa alitoa wito huo wakati akizungumza kufuatia kifo cha Rais Magufuli kilichotangazwa jana usiku na makamu wa Rais mama Samia Suluhu ambapo amesema kuwa wamepokea kwa mshituko mkubwa taarifa hizo lakini hwana budi kupokea kwani kazi ya Mungu haina makosa.
“Ninachoomba kwetu watanzania tukipokee lakini pia tumshukuru Mungu kwa huo muda aliotupa kuwa kiongozi wetu tuiombee familia yake imtazame Mungu na kumfanya awe faraja yao hivi sasa, Alisema Askofu Dkt Massangwa.
Alieleza kuwa kwasasa wanapaswa kuiombea nchi iendelee kuwa na amani na utulivu na kumuombea Makamu wa Rais ambaye ataapishwa kuwa Rais wa nchi kwa mujibu wa katiba ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania.
Alifafanua kuwa suala kubwa la kumuenzi ni kujitahidi kufuata nyayo zake pamoja na kwamba wao sio yeye lakini Mungu awasaidie na kuwapa utulivu ili waweze kumaliza maziko yake salama na kuendeleza yale aliyoyaadhisha
“Atakayepokea nafasi yake sio yeye hasa lakini Mungu amsaidie ampe amani, ampe utulivu ili aweze kukamilisha miradi ambayo ilishaanzishwa na mwelekeo ule ambao ulikuwa unaipeleka nchi yetu katika kuimarisha uchumi uchumi wa kati, Alisema Askofu Dkt Massangwa.