*******************************************
Na Allawi Kaboyo – Bukoba.
Mkoa wa Kagera umeungana na mikoa mingine nchini katika uzinduzi wa maadhimisho ya wiki ya maji kwa kutembelea miradi mbalimbali inayotekelezwa na serikali pamoja na kupanda miti rafiki kwenye vyanzo vya maji ambapo wananchi wamehusiwa kulinda vyanzo hivyo.
Katika taarifa iliyotolewa na meneja wa wakala wa maji na usafi wa mazingira vijijini Ruwasa Mhandisi Warioba Sanya imeeleza kuwa katika kipindi cha serikali ya awamu ya tano chini ya Rais John Pombe Magufuli, Mkoa wa Kagera umeweza kutekeleza miradi mikubwa ya maji yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 263 ambayo haijawahi kutokea kwenye awamu zote za uongozi zilizopita.
Mhandisi Sanya amesema kuwa katika kipindi cha miaka mitano wameweza kujenga miradi ya maji 70 vijijini na tayari imekemilika na inatoa huduma kwa wananchi, huku miradi 65 ikiendelea kujengwa huko vijiji ili kurahisisha upatikanaji wa maji kwa ukaribu.
“Wakati tunaadhimisha hii wiki ya maji sisi kama wahandisi wa Mkoa wa Kagera tunajivunia kutekeleza miradi mikubwa na yenye tija kwa wananchi wetu, tangu kuumbwa kwa dunia hii uwekezaji mkubwa tena kwenye sekta ya maji haujawahi kufanyika hivyo tunaungana na wananchi wa mkoa wa Kagera kuishukuru serikali kwa hili.” Ameeleza Mhandisi Sanya.
Sanya ameongeza kuwa wao kama wataalamu hawatakuwa sababu ya kukwamisha upatikanaji wa maji kwa wananchi badala yake watahakikisha wananchi wa Kagera wanapata maji safi na salama na yenye kutosheleza kwa kuhakikisha wanatekelea miradi ya maji kwa ubora unaotakiwa.
Kuhusu suala la uharibifu wa miundombinu ya maji, Mhandisi Sanya amesema kuwa kumekuwepo na baadhi ya wananchi ambao sio wazalendo na wenye niao ovu ambao wamekuwa wakihujumu miundombinu ya maji, hali ambayo imekuwa ikiwasababishia hasara na kuleta usumbufu wa kutopatikana kwa huduma ya maji kwa wananchi wengine, ambapo ameongeza kuwa kutokana na sheria ya maji wamekuwa wakiwachukulia hatu wale wote waliokuwa wakibainika.
Kadole Kilugara katibu tawala wa wilaya ya Bukoba akiongea kwaniaba ya mkuu wa wilaya bukoba baada ya kutembelea miradi ya maji ya Bunena na Rubale amewashukuru watumishi wa idara ya maji Mkoani humo kwa jitihada kubwa wanazozifanya katika kuhakikisha wanawasogezea wananchi huduma ya maji karibu.
Kilugara amesema kuwa serikali inawekeza fedha nyingi kwenye miradi ya maji na mara nyingi miradi hiyo imekuwa ikiishi kwa muda mfupi na kuacha kutoa huduma kwa wananchi hali iliyokuwa ikipelekea wananchi kutokuwa na imaani na serikali yao.
Ameongeza kuwa serikali haitamuonea haya mwananchi yeyote atakayebainika kuhujumu miundombinu ya maji kwa sababu zozote, amewataka wananchi kuwa walinzi namba moja wa miradi ya maji kwakuwa miradi hiyo ni yao, ambapo amezitaka pia kamati zamaji zinazoundwa kuhakikisha miradi inakuwa salama muda wote.
Akiongea kwaniaba ya wananchi watumia maji wa kijiji cha Rubale, Bi Aishati Saidi ameishukuru serikali kwa kufufua mmiradi ya maji iliyokuwa imekufa kwa kipindi kirefu na sasa inatoa huduma ya maji hivyo kuwapunguzia hadha ya kuhangaika kutafuta maji.
Kaulimbiu ya wiki ya miji ni “Thamani ya maji kwa uhai na maendeleo”