Mchanganyiko
29 minutes ago
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius John Ndejembi, amewataka Watanzania kuthamini juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati, huku akisisitiza uzalendo, uwajibikaji na matumizi sahihi ya fedha za umma ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija kwa Taifa. Makamu wa Rais ametoa wito huo mkoani Iringa wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi kwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la abiria na maegesho ya magari katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa, mradi unaotekelezwa kwa gharama ya zaidi ya shilingi bilioni 41. Amesema kukamilika kwa mradi huo kutaimarisha usafiri wa anga, kufungua fursa za kiuchumi na kuchochea ukuaji wa sekta ya utalii, hususan katika Hifadhi ya Taifa ya Ruaha. Aidha, amezitaka Wizara ya Uchukuzi, Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kutathmini uwezekano wa kuboresha miundombinu ya kiwanja hicho, ikiwemo uwekaji wa taa zitakazowezesha ndege kutua na kuruka wakati wa usiku. Katika hatua nyingine, Makamu wa Rais amewataka Watanzania kuunganisha nguvu katika ujenzi wa Taifa kwa kutambua wajibu wao badala ya kujiuliza Serikali imewafanyia nini, akisisitiza kuwa kila mmoja anapaswa kujiuliza amelifanyia nini Taifa lake. Amesema uwajibikaji na kufanya kazi kwa bidii kutaongeza tija, mapato ya Serikali na kuimarisha huduma za kijamii pamoja na miundombinu ya maendeleo. Akizungumzia usimamizi wa fedha za umma, amewataka mawaziri, viongozi wa taasisi, wabunge, wakuu wa wilaya, madiwani na watendaji wa Serikali katika ngazi zote kusimamia kikamilifu miradi ya maendeleo na kupambana na vitendo vya ubadhirifu na rushwa. Ameonya watu wanaodai asilimia ya fedha za miradi bila kufanya kazi yoyote, akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan haitawavumilia wabadhirifu na itahakikisha fedha za walipakodi zinatumika ipasavyo. Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhe. David Mwakiposa Kihenzile amesema Serikali imetenga takribani shilingi trilioni moja kwa ajili ya ujenzi na maboresho ya viwanja vya ndege katika mikoa ya Iringa, Njombe, Songea, Sumbawanga, Mwanza, Shinyanga, Manyara, Tanga, Mtwara, Lindi na Dodoma. Amesema utekelezaji wa miradi hiyo upo katika hatua mbalimbali, huku baadhi ikiwa imekamilika, mingine ikiendelea na mingine ikiwa katika hatua za maandalizi ya ujenzi na zabuni. Naye Waziri wa Ujenzi, Mhe. Masanja Kadogosa, akizungumzia kuchelewa mwa mradi wa barabara ya mchepuo wa Iringa, amesema mkandarasi aliyelipwa fedha za awali kwa ajili ya ujenzi wa kilomita 3.3 aliondoka eneo la mradi na kusababisha kazi kusimama. Amesema tayari ameitisha kikao na mkandarasi huyo ili kuhakikisha anarejea kazini, huku akiwaonya wakandarasi wanaoshindwa kutimiza wajibu wao kuwa wanaweza kuchukuliwa hatua, ikiwemo kufutiwa usajili na kuzuiwa kufanya kazi nchini. Awali, akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya mradi, Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta, amesema ujenzi wa jengo la abiria na maegesho ya magari katika Kiwanja cha Ndege cha Iringa unagharimu zaidi ya shilingi bilioni 41 na unatarajiwa kukamilika tarehe 30 Mei 2027. Amesema mradi huo ulioanza Julai 17, 2025, unatekelezwa na kampuni ya China Harbour Engineering Company Limited, huku kazi za ujenzi wa jengo la abiria na barabara za ndani zikiendelea. Besta amesema jengo hilo litakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria…