*******************************************
NA MWANDISHI WETU
MBUNGE wa Viti Maalumu Janeth Mahawanga, amesema anatarajia kuja na Mkakati wa Dira ya Maendeleo ya Kiuchumi kwa wanawake atakaouwasilishwa katika Kongamano la Siku ya Wanawake Duniani lililopangwa kufanyika Machi 13 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Gaudentia Kabaka anatarajiwa kuwa mgeni rasmi.
Kongamano hilo limeandaliwa na Mbunge huyo kupitia UWT , Mkoa wa Dar es Salaam na litafanyika katika Ukumbi wa Mlimani City.
Akizungumza, Jijini Dar es Salaam, Mbunge Janeth, alisema, wataitumia siku hiyo kupanga na kuwasirisha Dira ya Maendeleo ya Kiuchumi kwa Wanawake katika Mkoa wa Dar es Salaam chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.
“Kusudi ni kumfanya mwanamke ajiamini zaidi na kumkomboa kiuchumi, yeye, jamii yake na taifa kwa ujumla,”alisema Janeth.
Mbunge huyo alisema hafla hiyo itahusisha wanawake kutoka makundi mbalimbali, kama vile makundi ya watu wenye ulemavu, mabinti wa vyuo vikuu na kidato cha sita.
“Kwani ni muhimu kuwashirikisha pia mabiti ambao ni viongozi wa kesho ili kuwajengea uwezo sasa hivi na kuwafanya nao wajiandae kuwa wajasiriamali na wawekezaji ndani ya taifa lao, sambamba na kuwashirikisha katika masuala ya msingi yanayo mgusa mwanamke,”alibainisha.
Janeth alibainisha, siku hiyo kutakuwa na midahalo mbalimbali ambayo itahusu wadau na watalam wabobezi katika masuala yote yanayogusa shughuli za kumkomboa mwanamke kiuchumi hasa kwa kuzingatia serikali inapambana kuhakikisha wanawake na vijana wanamiliki viwanda ambavyo vitakuwa mkombozi kwenye jamii yetu,”salibainisha Mbunge huyo.
Alitaja mambo ya msingi yatakayo jadiliwa ni kukutana na wadau, tasisi na mashirika yanayojiuhisha na masuala ya kuwezesha wanawake kiuchumi.
“Kuzitambua shughuli za taasisi hizo na jinsi ya kupata fursa kutoka kwa wadau hao. Kupeana maarifa ya kumkomboa mwanamke kifikra, kijamii na kiuchumi kupitia UWT na jinsi ya kumshirikisha mwanamke katika uchumi wa viwanda vidogo, ujasirimali na afya,”alifafanua.
Mambo mengine ni masuala yote yanayo husu elimu ya ujasiriamalim usafi wa mazingira na kuzitambua haki za msingi za kisheria ambazo mwanamke huwa anakosa kwa kuto kuzijua hasa katika kumiliki ardhi, mirathi, mali na malezi ya watoto
“Pia namna ya kuzitambua fursa zinazotuzunguka ndani na nje ya mkoa wa Dar es Salaam, ambazo zitatuongezea vipato na kuimarisha uchumi wetu. Aidha kupata fursa ya kuwakutanisha wanawake waliofanikiwa,”alifafanua Janeth.
Kauli mbiu ya Siku bya Wanawake Duniani ambayo Kilele chake ni leo ni Wanawake katika uongozi: Chachu kufikia Dunia yenye usawa.
Siku ya Wanawake Duniani chimbuko lake ni mwaka 1911 kufuatia maandamano ya wanawake wafanyakazi wa sekta za viwanda nchini Marekani waliokuwa wakipinga mazingira duni ya kazi, unyanyasaji wa kijinsia na maslahi madogo.