Baadhi ya wazee wilayani Kaliua wakimsikiliza janai Mbungewa Jimbo la Kaliua Aloyce Kwezi wakati akitoa shukurani kwa wananchi kwa kumchagua.
Mbunge wa Jimbo la Kaliua Aloyce Kwezi akiwa katika mkutano jana na wazee kwa lengo la kuwashukuru kwa kumchagua yeye kuwa Mwakilisha wao Bungeni na kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwa ajili kuwaongoza tena kipindi kingine.
NA TIGANYA VINCENT
WAKAZI wa Wilaya ya Kaliua wameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuwapelekea kiasi cha shilingi bilioni 3.3 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya afya na elimu.
Fedha hizo zilitolewa Desemba ni kwa ajili ya uendelezaji wa ujenzi wa majengo katika Hospitali ya Wilaya, kusadia sekta ya elimu ya msingi na Sekondari na kusaidia mpango wa kunusuru kaya maskini unaoratibiwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii(TASAF).
Taarifa hiyo ilitolewa jana na Mbunge wa Jimbo la Kaliua Aloyce Kwezi wakati mkutano na wazee kwa lengo la kuwashukuru kwa kumchagua yeye kuwa Mwakilisha wao Bungeni na kumchagua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt John Pombe Magufuli kwa ajili kuwaongoza tena kipindi kingine.
Alisema kupatikana kwa fedha hizo kutawasaidia kuharakisha kukamilika kwa Hospitali ya Wilaya na kuwawezesha kupata huduma katika mazingira yao.
Kwezi aliongeza kuwa Hospitali hiyo ni muhimu kwao kwa kuwa itasaidia kuwaondolea adha ambazo wakinamama wajawazito walikuwa wakizipata ikiwemo kutozwa fedha kwa ajili ya glovu wanapokwenda kujifunga na kutozwa gharama kubwa wanapohitaji damu na wazee kuambaiwa kuwa hakuna dawa wanapokwenda kutibiwa katika Hospitali binafsi.
Katika kutekeleza ahadi mbalimbali alizotoa ,Kwezi alisema kwa upande wake ameshatoa kiasi cha shilingi milioni 70 kutoka Mfuko wa Jimbo ambazo amezipeleka katika Kata zote wa ajili ya shughuli mbalimbali za maendeleo ya wananchi.
Alisema ataendelea kukutana mara kwa mara na wananchi kusilikiza kero na matatizo yao mbalimbali na kuyatafutia ufumbi ili yasije yakawa kiwazo katika maendeleo yao.
Kwezi alisema katika kipindi alichokutana na kundi la wazee amebaini kuwepo kwa kero nyingi ikiwemo wazee kukosa dawa wanapokwenda kutibiwa , wakimama wajawazito kuamuliwa kununua vitu ambavyo havipo katika miongozo ya Wizara ya afya na ndugu wa wagonjwa kutozwa kiasi kingi cha chupa za damu kuliko anachohitaji mgonjwa.
Alisema anapanga kukutana na Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji kwa ajili ya kupanga mpango wa kuwaandaa wataalamu ili waweze kujibu na kutafutia ufumbuzi chamngamoto hizo kwa wakati.
Aidha Mbunge huyo aliishukuru Serikali ya Awamu ya Tano kwa kuanzisha mradi wa upelekaji maji ya ziwa Victoria kupitia Urambo.
Alisema tayari wataalamu wameshafika wilayani humo na wakati wowote utekelezaji wa ujenzi wa mradi huo utaanza na kuongeza kuwa kukamilika kwa mradi kutaongeza fursa za uwekezaji katika sekta ya kilimo na ufugaji
Katika hatua nyingine Kwezi alisema ataendelea kuhamasisha suala na michezo katika vijiji na mashule kwa lengo la kuibua vipaji.
Alisema hatua hiyo itasaidia vijana wengi kupata fursa za ajira kupitia sekta hiyo na kuitangaza vema Wilaya ya Kaliua ndani na nje ya Tanzania.
Kwezi alisema hadi hivi sasa ameshakwisha kutoa vifaa mbalimbali vya michezo kwa vijiji vyote vya Jimbo lake na awamu inafuata ni kupeleka mashuleni.