Home Mchanganyiko SERIKALI YATUMIA ZAIDI YA MILIONI 664 KAMA MALIPO YA KAYA MASKINI TUNDURU

SERIKALI YATUMIA ZAIDI YA MILIONI 664 KAMA MALIPO YA KAYA MASKINI TUNDURU

0

Mratibu wa mfuo wa maendeleo ya jamii Tasaf wilaya ya Tunduru Muhidin Shaibu akiongea jana na wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini wa kijiji cha Nalas kata ya Nalasi kabla ya kuanza kwa zoezi la malipo ya ruzuku ya mwezi Novemba na Desemba 2020 ambapo  zaidi  ya shilingi milioni 664 zimelipwa kwa wanufaika wa mpango huo wilayani Tunduru. Mwezeshaji wa Tasaf kijiji cha Nalasi Aziz Taus akizungumza  na walengwa wa mpango wa kunusuru kaya maskini katika kijiji hicho ambapo aliwataka kutumia kiasi cha fedha wanazopata kujiunga na Bima ya Afya.

Picha na Muhidin Amri,

***************************

 Na Muhidin Amri,
Tunduru

MFUKO wa maendeleo ya Jamii TASAF katika wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma,umetumia jumla ya shilingi  664,288,000.00 kama malipo ya walengwa 12,785 kutoka vijiji 88 waliopo kwenye mpango wa kunusuru kaya maskini wilayani humo.

Hayo yamesemwa jana na Mratibu wa Tasaf wilayani Tunduru Muhidin Shaibu wakati wa zoezi la malipo ya  walengwa waliopo kwenye mpango huo katika vijiji vya Lipepo na Nalasi ikiwa ni malipo ya mwezi Novemba na Desemba 2020.

Aidha, amewataka wanufaika  hao kutumia vizuri fedha za ruzuku wanazopata kwa kuanzisha na kuendeleza miradi badala ya kutumia  katika anasa ili kuepuka kuendelea kutegemea ruzuku ya Serikali ambayo inatolewa kila baada ya miezi 2.

Shaibu amewakumbusha walengwa na wanufaika wa mpango huo  kutumia ruzuku wanazopata kwa usahihi,kuendelea kuhamasishana kujiunga na mfuko wa Bima ya Afya iliyoboreshwa ambapo hadi sasa jumla ya kaya 2620 zimeshajiunga na mfuko huo.

Kwa mujibu wake, mbali na zoezi la malipo ya fedha hizo TASAF imeendelea kuhakiki  mashuleni uwepo wa watoto wanaotoka katika kaya maskini wakiwa na vifaa vya shule kama sale na madaftari lengo ni kujiridhisha kama mzazi au mlezi anatimiza wajibu wake kutokana na ruzuku wanazopokea.

Alisema,hatua hiyo itasaidia sana kuepuka adhan a migogoro ya kisheria inayoweza kuwakumba watoto na wazazi wao wakati wa ukaguzi wa maendeleo yao shuleni pamoja na wale wanaotakiwa kuhudhuria kliniki.

Kwa upande wake mwezeshaji wa Tasaf katika kijiji cha Nalas Aziz Tausi  alisema katika kijiji hicho zaidi  ya shilingi milioni 4.836 zimelipwa kwa walengwa kama ruzuku ya mwezi Novemba na Desemba.

Alisema, malipo hayo yamekwenda sambamba na uhakiki wa taarifa za wanafunzi waliomaliza elimu ya msingi mwaka 2020 na kujiunga na  kidato cha kwanza katika mwaka wa masomo 2021  wanaotoka kaya maskini.

Amewakumbusha walengwa kuzingatia kanuni na taratibu za Tasaf kwa kipindi chote cha mradi  kwa kuwa kuna fursa nyingi ambazo Serikali inaendelea kuzitoa kwa kaya hizo.

Alisema, dhamira kubwa ya Serikali ni kuona kaya za walengwa zinaondokana na umaskini uliokithiri na kuwa kaya zenye uwezo wa kujitegemea kwa mahitaji yote muhimu badala ya kuendelea kusubiri na kupokea ruzuku ya Serikali inayotolewa na Tasaf.

Mwezeshaji wa Tasaf kijiji cha Lipepo Elienea Mndeme alisema, katika kijiji hicho  zaidi ya shilingi milioni  2.912 zimetolewa kama ruzuku kwa walengwa wa mpango huo.

Baadhi ya wanufaika wa mpango huo Rajabu Mussa na Abdala Said  wameishukuru Serikali kuendelea kutoa ruzuku kwao kwani itawasaidia sana kuboresha hali za maisha na kuhaidi kutumia vizuri fedha hizo kujiimarisha kimaisha na kujiunga na Bima ya Afya kama Serikali inavyowataka.