Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert akitoa hotuba yake Katika Kikao cha Mwaka cha Kamati ya Ushauri wa Mkoa Shinyanga mapema jana.
Katibu Tawala Msaidizi Mipango na Uratibu Mkoa wa Shinyanga Bw. Joakim Otaru akitoa mada yake Katika Kikao cha Mwaka cha Kamati ya Ushauri wa Mkoa Shinyanga mapema jana.
Baadhi ya Wajumbe wa Kamati ya Ushauri wa Mkoa Shinyanga wakifuatilia jambo katika kikao cha mwaka cha ushauri wa Mkoa jana Mkoani Shinyanga.
……………………………………………………………………………………….
na mwandishi wetu Shinyanga
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga Bw. Albert Msovela amewataka Wakulugenzi wote wa Halmashauri za Shinyanga kuhakikisha wanafunzi wote waliopangiwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka huu wanaripoti shuleni kama inavyotakiwa ifikapo Machi 1, mwaka huu.
Akitoa hotuba yake Katika Kikao cha Mwaka cha Kamati ya Ushauri wa Mkoa kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainab Telack, Bw. Msovela alisema kuwa idadi ya wanafunzi ambao hawajaripoti Shuleni kwa takwimu zilizopo ni 7,416 ambao ni sawa na 25%.
Aidha Bw. Msovela aliitaja idadi ya wanafunzi waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza Mkoa wa Shinyanga kuwa 26,2017 na kati ya hao wavulana ni 12,360 na wasichana ni 13,857 na kati ya hawa wavulana waliofika shuleni ni 19,776 ambao ni sawa na 75%.
Aidha Bw. Msovela aliongeza kuwa idadi ya wavulana ambao wameisharipoti shuleni ni 9,718 na wasichana ni 10,058 kwa takwimu hizo idadi ya wanafunzi ambao hawajaripoti ni kubwa na hivyo kutoa wito kwa Mamlaka zote za Halmashauri na wadau wote wa serikali kuhakikisha watoto wote wanaripoti shuleni kama ilivyopangwa.
Aidha Bw. Msovela amewataka Wakulugenzi pia kuhakikisha wanakamilisha ujenzi wa vyumba vya madarasa ambavyo ni takribani 142 kwa kuzingatia viwango bora ambavyo vinaendana na thamani ya fedha iliyotolewa na kuongeza kuwa vyumba hivyo viko katika hatua mbalimbali za ukamilishaji.
Aidha Bw. Msovela ametaka vyumba vya madarasa kukamilika ifikapo Februari 25 mwaka huu kwani hivi sasa kuna mwitikio mkubwa wa wanafunzi kuanza shule kufutia fursa iliyopo ya sera ya elimu bure na kuwataka wadau wote nchini kuchangia katika utengenezaji wa madawati ili kupambana na changamoto ya upungufu wa madawati.
‘’Ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa miundombinu ya madawati ambayo ni takribani 1,000, viti, meza pamoja na madarasa na wito kwa wadau wetu walio ndani na nje ya mkoa wetu kuchangia utengenezaji wa madawati na madarasa ili kukabiliana na changamoto hii inayozidi kujitokeza.’’Aliongeza Bw. Albert Msovela Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga.
Kikao cha kamati ya ushauri Mkoa kilishikirikisha wadau mbalimbali wa serikali mkoani Shinyanga ambao pia waliwasilisha mipango na mikakati iliyopo ya utendaji kazi ikiwemo changamoto zilizopo kwa lengo la kuwezesha Mkoa kutoa huduma bora kwa wananchi.