![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/02/AA-1-1024x768.jpg)
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/02/S-1024x768.jpg)
![](https://fullshangweblog.co.tz/wp-content/uploads/2021/02/Q-1024x768.jpg)
………………………………………………………………………………
Na.Faustine Gimu Galafoni.
Baadhi ya wananchi katika kijiji cha Sungamile Halmashauri ya Msalala Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga wameiomba serikali kuwasogezea huduma ya Mawasiliano hususan mnara katika kijiji hicho.
Wakizungumza na mtandao huu Juma hili kijijini hapo baadhi ya wananchi walisema mawasiliano ya simu yamekuwa ya kusuasua katika kijiji hicho hali ambayo husababisha kupanda juu ya miti au juu ya barabara ili waweze kuwasiliana.
Nkwabi Ndizu ni mmoja wa wakazi wa Sungamile ambapo alisema chanzo cha mawasiliano ya Simu kusuasua katika eneo hilo ni minara ya simu kuwa mbali ambapo hutegemea minara ya mawasiliano kutoka mji wa Kagongwa ,Isaka na mnara wa Igusule uliopo Wilaya jirani ya Nzega mkoani Tabora .
“Kwa kweli suala la mawasiliano katika kijiji hiki limekuwa changamoto kubwa tunapotaka kuwasiliana na ndugu na jamaa inatulazimu kusimama barabarani kwenye mwinuko hali ambayo inaweza kusababisha ajali kama unavyojua barabara hii ni kubwa yanapita magari mbalimbali ya kwenda nje ya nchi ikiwemo Rwanda,Burundi,Congo DRC,pia wakati mwingine inatulazimu kupanda juu ya miti tunachoomba ni mnara wa mawasiliano utufikie wana Sungamile”alisema.
Naye Lucas Lumwecha alifafanua kuwa chanzo kingine cha Mawasiliano ya simu kusuasua katika kijiji hicho ni kuwa bondeni huku Saida Yagoda akieleza kuwa kutokana na mawasiliano kuwa ya chini panaweza kujitokeza madhara mbalimbali ikiwemo husababisha vifo kwani pindi panapokuwa na mgonjwa huwezi kupiga simu ili kuokoa maisha.
Masanja Makelemo Mabula ni Kiongozi wa Kitongoji cha Igalula kijiji cha Sungamile Wilayani Kahama Mkoani Shinyanga alisema masuala ya Mawasiliano hususan internet na kupiga simu ni shida katika kijiji hichoi.
“Wakati mwingine una mgonjwa unatafuta daladala network ni shida haisomi ni kilio kikuu katika eneo letu”alisema.
Castory Gwalila Kilio kikuu kwake ni pale anapojiunga kifurushi lakini mtandao haupatikani mwishowe muda unaisha kutokana na mawasiliano kusuasua .
“Wakati mwingine tunajiunga na vifurushi vinaisha tu maana network haipatikani na pia tunapokimbilia barabarani kutafuta network kunaweza kusababisha ajali mfano matairi ya magari yanaweza kufyatuka “alisema.
Naye Shija Mihambo ambaye ni kondakta wa mabasi yaendayo mikoani ambapo alifafanua kuwa pindi anapotafutwa na wateja akiwa katika kijiji hicho simu huwa hazipatikani huku Ismail Mipawa akiomba huduma za mawasiliano kuboreshwa zaidi.
Marco Itenga ni Afisa Mtendaji wa kijiji cha Sungamile akifanya mahojiano maalum na mtandao huu alikiri kuwepo kwa changamoto ya Mawasiliano katika kijiji hicho ambapo alisema
“Hata Ofisini kwetu ninapofika katika kijiji hiki huwa inanilazimu kutoka ofisini kutafuta eneo zuri la mtandao kwa ujumla mawasiliano kwetu ni mwiba na tuna zaidi ya kaya 500 na zaidi ya wakazi 3000 katika kijiji hiki wanahangaika katika suala zima la mawasiliano”alisema.
Kama ilivyo changamoto ya Mawasiliano katika kijiji cha Sungamile Kahama ,eneo la Mbulu mkoani Manyara nalo linachangamoto kama hiyohiyo Februari 10,2021 Bungeni jijini Dodoma mbunge wa Mbulu vijijini Flatei Grigory Massay alihoji ni lini Serikali itajengwa minara ya simu katika kata za Endahagichen-Ndamilay,Mewadan-Magong na Endaghadat -Qamtananat katika jimbo la Mbulu vijijini Mkoani Manyara ambazo hazina mawasiliano.
Akisimama kwa mara ya kwanza bungeni tangu ateule kuwa Naibu Waziri wa Wizara mpya ya “Mawasiliano na Teknolojia ya Habari”Kundo Mathew alisema mpaka sasa kata 633 zilikwishapata huduma ya mawasiliano huku kata 361 ujenzi ukiendea nchi nzima kwa ruzuku ya serikali na mwezi huu serikali inatarajia kutangaza zabuni zingine awamu ya 6 kufikisha huduma ya mawasiliano katika kata 74 zenye vijiji 206 kote nchini .
Hata hivyo,Naibu Waziri Mathew alisema pamoja na jitihada za serikali ,bado kuna takriban kata 1365 kati ya kata 3956 zilizopo Tanzania bara na Wadi 16 kati ya wadi 111 zilizoko Zanzibar bado zina changamoto ya upatikanaji huduma ya mawasiliano ambapo serikali kupitia mfuko wa mawasiliano kwa wote [UCSAF] inafanya tathmini ili vijiji vyote viingizwe katika kutangaza tenda ya zabuni mwezi huu.