Wakazi wa Tanga waliojitokeza katika kampeni maalum ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi pamoja na saratani ya tezidume wakisikiliza jambo kwa makini kutoka kwa mtaalamu.
Wakazi wa Tanga waliojitokeza katika kampeni maalum ya uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi pamoja na saratani ya tezidume wakisikiliza jambo kwa makini kutoka kwa mtaalamu.
Mtaalamu Mbobezi Masuala ya Afya ya Jamii kutoka Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI),Johnson Katanga akitoa elimu kwa umma kuhusu saratani ya tezidume
………………………………….
Na Mwandishi Maalum (ORCI)– Tanga
Wanawake wamehimizwa kuzingatia uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi hata kama wameacha kujamiana maishani mwao na hata kama hawakuwahi kukutwa na mabadiliko ya awali ya saratani hiyo katika uchunguzi uliopita.
Rai hiyo imetolewa leo na Muuguzi Mkuu wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Jesca Kawegere alipokuwa akijibu swali la mwanamke (jina linahifadhiwa) aliyejitokeza katika kampeni ya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi inayofanyika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo.
Mama huyo ambaye alitaja wazi kwamba yeye ni mwathirika wa Ukimwi, alihoji kuna umuhimu gani kuendelea kufanya uchunguzi wa awali ikiwa katika uchunguzi aliowahi kufanyiwa mara kadhaa hakukutwa na mabadiliko yoyote na sasa ameacha kujamiiana.
“Nazingatia matumizi ya dawa za ARVs, nimechunguzwa mara kadhaa saratani ya mlango wa kizazi, sijakutwa na mabadiliko ya awali, nimeacha kujamiiana, Je! bado kuna sababu za mimi kuendelea kuchunguzwa saratani hiyo,? Alihoji.
Akijibu swali hilo, Muuguzi Mkuu wa ORCI, Kawegere amesema “Ni muhimu kuendelea kufanya uchunguzi wa awali wa saratani ya mlango wa kizazi hata kama mwanamke ameacha kujamiiana.
“Kwa sababu ni vigumu kujua, kubaini lini kirusi cha Human Papilloma (HPV) kinachosababisha ugonjwa huo kitaleta mabadiliko katika mwili wake na hatimaye kuleta athari kubwa endapo hakitagundulika mapema,” amesema.
Amesema kirusi cha HPV huweza kukaa ndani ya mwili wa mwanamke hata kwa miaka 10 na kuanza kuonesha athari na ndiyo maana wanahimiza uchunguzi wa awali mara kwa mara.
Akitoa elimu kuhusu saratani ya tezidume, Mtaalamu Mbobezi Masuala ya Afya Jamii wa Taasisi ya Saratani Ocean Road (ORCI), Johnson Katanga, amehimiza wanaume hasa wenye umri kuanzia miaka 40 na kuendelea kujenga utamaduni wa kuchunguza saratani hiyo mara kwa mara.
“Sasa hivi tuna kipimo cha damu, kama vile unavyochunguzwa malaria, kipimo hicho kinatuwezesha wataalamu kufanya uchunguzi wa awali wa saratani ya tezidume, msiogope,” ametoa rai.
Wananchi waliojitokeza kwenye uchunguzi huo ambao leo ni siku ya pili, wameshukuru wataalamu wa ORCI pamoja na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Tanga – Bombo kwa kuwafikisha huduma hiyo rafiki.
Wataalamu wa ORCI wamepiga kambi maalum ya uchunguzi wa awali wa saratani ya kizazi kwa wakazi wa Tanga, kambi hiyo iliyoanza Januariu 28, 2021 inayotarajiwa kukamilika Januari 30, 2021 imeenda sambamba na utoaji wa mafunzo kwa watoa huduma za afya zaidi ya 25 wa Mkoa huo.