*Afurahishwa na ubunifu wa wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Ufundi Ifunda
WAZIRI MKUU, Kassim Majaliwa amesema Serikali inaandaa bajeti kwa ajili ya awamu ya pili ya ukarabati wa shule kongwe nchini ambao utahusisha nyumba za walimu pamoja na majengo mengine kwa lengo la kuwawezesha watumishi hao kuishi katika mazingira bora na kutekeleza majukumu yao ipasavyo.
Pia, Waziri Mkuu amesema amefurahishwa na ubunifu wa kutengeneza vitu mbalimbali uliooneshwa na wanafunzi wanne wa shule ya Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Ufundi na kwamba suala hilo ni moja kati ya jambo muhimu linalosisitizwa na Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Ameyasema hayo leo (Jumapili, Januari 24, 2021) baada ya kupata taarifa ya ukarabati na kukagua miundombinu ya majengo ya Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ifunda na Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Ufunda zilizopo Halmashauri ya Iringa Vijijini. Amesema amefurahi kuona mazingira ya shule yakiwa yamebadilika baabda ya ukarabati.
Amesema ameridhishwa na ukarabati uliofanyika katika shule hizo na kwamba Serikali itaendelea kuimarisha mazingira ya utoaji wa taaluma nchini ikiwa ni pamoja na kuboresha miundombinu na kuongeza idadi ya walimu katika shule zenye upungufu, hivyo amewataka waendelee kuwa na subira wakati suala hilo likishughulikiwa.
Kuhusu ukarabati wa shule kongwe nchini, Waziri Mkuu amesema hayo ni matokeo ya ahadi zilizotolewa na Rais Dkt. Magufuli mwaka 2015 na kwamba Serikali itahakikisha ahadi zote zilizoahidiwa kwa Watanzania zitatekelezwa kwa kiwango kikubwa kama ilivyofanywa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.
Kadhalika, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wanafunzi wasome kwa bidii na waachane mwelekeo wa kujidharau na kujiona kwamba hawawezi jambo ambalo wanaweza kulifanya kwani si sahihi kwa kuwa Watanzania wanauwezo mkubwa wa kuzisimamia rasilimali za Taifa kwa maendeleo yao.
Amesema Serikali inasomesha wanafunzi kwa lengo la kuwaandaa ili waweze kuwa wasimamizi wazuri wa rasilimali za Taifa, hivyo amewasihi wasome kwa bidii na walimu waendelee kufanyakazi zao vizuri kwa kuzingatia weledi. Serikali inatambua mchango mkubwa wanaoutoa katika maendeleo ya Taifa.
Shule za Sekondari zilizokarabatiwa katika mkoa wa Iringa ni Shule ya Sekondari ya Wasichana ya Ifunda, Shule ya Sekondari ya Ufundi ya Ifunda, Shule ya Sekondari ya Tosamaganga, Shule ya Sekondari ya Malangali, Shule ya Sekondari ya Lugalo na Shule ya Sekondari Iringa kwa gharama ya shilingi bilioni 7.8.
Akizungumzia kuhusu ubunifu wa vifaa mbalimbali uliofanywa na wanafunzi hao, Waziri Mkuu amesema Serikali imejipanga kuendeleza ubunifu huo ili uweze kuleta manufaa kwa wananchi na Taifa kwa ujumla. “Wanafunzi hawa washiriki katika maonesho ya ubunifu ili watu wajue kuwa Tanzania kuna vijana wenye uwezo wa kubuni vitu mbalimbali na si kutegemea kutoka mbali.”
Wanafunzi hao ni Elia Mkumbo aliyebuni kifaa maalumu kwa ajili ya kuwasaidia watu wasioona ambacho ninatoa sauti ya kumuwezesha kugundua kama mbele yake kuna kitu chochote (Blind Assistant), pia mwanafunzi huyo amesema anatarajia kuendeleza ubunifu wake kwa kutengeneza kifaa kitakachounganishwa na macho ili kumuwesha asiyeoona kuona.
Wengine ni Oscar Herman aliyebuni kifaa maalumu kinachomuweza kugundua hitilafu ya umeme kabla ya kutokea (Local Connection Detector), Japhet Danford amebuni kifaa kinachomuwezesha mtu kwa mfano, kuwasha mfumo wa umwagiliaji kwa kutumia simu ya mkononi hata kama yuko mbali na eneo la shamba (Tele Switch) na Dhuwaiya Latwif amebuni kifaa kinamuwezesha mtu kubaini ujazo wa maji kwenye tanki bila ya kuchungulia (Water Level Indicator)
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Hapi amesema anaishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya ukarabati wa shule hizo ambazo awali zilikuwa katika hali mbaya na majengo yalikuwa yamechoka hivyo kuwaondolea wanafunzi morari ya kusoma na morari ya kufundisha kwa upande wa walimu.
“Tunamshukuru sana Rais Dkt. Magufuli kwa uamuzi wake wa busara wa kuamua kutoa fedha kwa ajili ya kuzikarabati shule kongwe nchini na mkoa wa Iringa pekee ulipewa shilingi bilioni saba kwa ajili ya ukarabati wa shule kongwe. Leo nasimama kwa fahari mkoa wetu umeshika nafasi ya pili Kitaifa katika matokeo ya kidato cha pili na matokeo ya kitato cha nne tumeshika nafasi ya tatu Kitaifa na shule za Serikali ndio zimetubeba.”
Awali, Waziri Mkuu alizindua zoezi la upandaji miti katika Chuo cha Mafunzo ya Uongozi chaa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Ihemi na kisha kukagua kitalu nyumba na kiwanda cha ushonaji nguo. Pia, Waziri Mkuu alitembelea Shule ya Sekondari ya Lyandembela na kuzungumza na wananchi, wanafunzi na walimu baada ya kupokea taarifa ya mwenendo wa madarasa katika shule hiyo.