Home Mchanganyiko RC WANGABO AWATAKA WANANCHI KUITUMUA WIKI YA SHERIA ILI KUPATA ELIMU ZAIDI

RC WANGABO AWATAKA WANANCHI KUITUMUA WIKI YA SHERIA ILI KUPATA ELIMU ZAIDI

0

Baadhi ya waandamanaji wakiingia katika eneo rasmi liliondaliwa kwaajili ya hafla fupi ya ufunguzi wa wiki ya sheria nchini kwa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga wakiwa wamebeba bango lenye kauli mbiu ya Wiki hiyo ya Sheria.

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo akitoa nasaha zake katika ufunguzi wa Wiki ya Sheria nchini katika viwanja vya Mandela Mjini Sumbawanga.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akisalimiana na Kaimu Jaji Mfawidhi wa Makama kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga Mh. Cyprian Mkeha muda mfupi baada ya mkuu huyo wa mkoa kufungua wiki hiyo ya Sheria.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (kushoto) akisikiliza maelezo ya Afisa wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rukwa (TAKUKURU) mkoani Rukwa Emanuel Mtuka wakati wa ukaguzi wa huduma za elimu zinazotolewa na Taasisi mbalimbali katika viwanja hivyo.

Mkuu wa Mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo (waliokaa katikati) katika picha ya Pamoja na waheshimiwa mahakimu na majaji wastaafu na baadhi ya wajumbe wa kamati ya ulinzi na usalama mkoa.

…………………………………………………………………………..

Mkuu wa mkoa wa Rukwa Mh. Joachim Wangabo amewataka wananchi mkoani humo kuhakikisha wanafika katika mabanda ya kutolea elimu ya sheria ili kuitumia fursa ya kupata elimu hiyo inayotolewa bure kwa kipindi cha wiki nzima ya sheria.  

Mh. Wangabo amesema kuwa elimu hiyo inayotolewa na Mahakama Pamoja na wadau wengine ikiwemo Mawakili wa Kujitegemea, Serikali, Jeshi la Polisi, Ofisi ya Mkurugenzi wa uendeshaji wa Mashataka (DPP), Ofisi ya Wakili (Solicitor General), Baraza la Ardhi Pamoja na Taasisi mbalimbali itawawezesha wananchi hao kuona njia za kutatua migogoro mbalimbali.

Amesema kuwa wananchi wamekuwa na malalamiko na migogoro mingi inayohusu mambo ya kisheria na hawajui sheria na hivyo kuwataka kuitumia wiki hiyo ya sheria iliyoanza tarehe 23.1.2021 kupata ushauri katika changamoto mbalimbali za kisheria wanazokabiliana nazo katika kutafuta haki zao.

“Elimu ni ya Bure itumieni hapa, kwa wale ambao watashindwa kufika hapa, wasikilize vyombo vya Habari, wasome magazeti, wafuatilie kule, kuna elimu ya bure ambayo inatolewa wiki nzima hii, tusikilize redio, watumishi wa mahakama wamejipanga, mahakimu majaji wanatoa elimu kule ya bure na wakati mwingine kutakuwa na mawasiliano ya moja kwa moja, unauliza swali lako utajibiwa.”

“Naona watu wengi sana wanamsumbua Mkuu wa Wilaya wakifikiri yeye ndio hakimu yeye ndio Jaji, yeye ndio mwanasheria, mtu anadhani akienda kule migogoro yake yote inaishia kule, sikilizeni fuatilieni vyombo vya Habari, ili muweze kujua masuala ya kisheria, si kila jambo linatatuliwa na mkuu wa Wilaya, Mkuu wa mkoa, Sisi tunafanya upatanishi ili watu waridhiane tu basi, lakini ukitaka haki ni mahakamani,” Alimalizia.

Mh. Wangabo ameyasema hayo wakati akifungua wiki ya sheria nchini leo tarehe 24.1.2021 kwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga, wiki ambayo imeambatana na matukio ya kutembea umbali wa kilomita 9 pamoja na maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwa Mahakama Kuu nchini.

Aidha, Mh. Wangabo ametumia nafasi hiyo kuipongeza Mahaka kuu ya Tanzania kwa kuadhimisha miaka 100 (karne moja) tangu kuanzishwa kwake mwaka 1921 huku akiwashauri kutafakari kwa kina mambo yanayotakiwa kuboreshwa ili kuendelea kudumisha Amani, Uhuru, Udugu na Haki kwaajili ya ustawi wa nchi yetu.

Wiki hii ya Sheria inaongozwa na kauli mbiu ya miaka 100 ya Mahakama kuu nchini isemayo; “Mchango wa Mahakama katika nchi inayozingatia Uhuru, Haki, Udugu, Amani na Ustawi wa Wananchi 1921 – 2021”.