………………………………………………………………………………….
Na. Damian Kunambi, Njombe.
Ikiwa ni muendelezo wa ziara ya mbunge wa jimbo la Ludewa Joseph Kamonga ya kutembelea wananchi pamoja na shule mbalimbali na kusikiliza changamoto zao, wakazi wa kata ya Ludewa wamemuomba mbunge huyo kuwatatulia tatizo la barabara kuelekea mashambani ili kuweza kusafirisha mazao yao kwa urahisi hasa barabara ya Nganda ambako ndiko kuna wakulima wengi zaidi.
Wakizungumza na mbunge huyo katika mkutano wa hadhara wananchi hao wamedai kuwa wamekuwa wakipita tabu jinsi ya kusafirisha mazao yao pindi wanapovuna kwani barabara iliyopo hairuhusu magari kufika kwa urahisi kitu ambacho husababisha kushindwa kuwa na wakati mgumu.
Aidha mbunge huyo papo kwa hapo alimsimamisha Mhandisi wa wakala wa barabara za vijijini na mijini (TARURA) wa wilaya hiyo Butene Jilala ili kutolea majibu juu ya hoja hiyo ambapo amesema kuwa barabara hiyo ya Nganda tayari imekwisha ingizwa kwenye bajeti ya sasa hivyo mwakani wananchi hao watarajie kuanza kwa ujenzi huo.
Ameongeza kuwa katika maeneo mengine ya mashambani amewaomba wananchi kuruhusu TARURA kuwatengenezea barabara pasipo kudai fidia kwakuwa mara nyingi wanapohitaji fidia hizo huleta mlolongo mrefu unaopelekea kuchelewa kwa ujenzi huo.
“Wananchi mnapodai fidia pale inapohitajika kupitisha barabara katika mashamba yenu hupelekea kuchelewa kwa Maendeleo kwani tutalazimika kuchukua muda mrefu kwa ajili ya hatua mbalimbali za ulipaji wa fidia hizo hivyo nawasihi kama mnauhitaji sana na barabara hizi basi wekeni pembeni masuala ya fidia kwa wakati huu”, Alisema Jilala.
Sambamba na changamoto hiyo ya barabara mashambani wananchi hao pia walitoa changamoto zao nyingine ikiwemo kutengenezewa kituo cha mafuta kwakuwa kilichopo hakikidhi mahitaji yao, kukatika katika kwa umeme, michango mashuleni, mipango miji na nyinginezo ambapo mbunge huyo alizichukua changamoto hizo na kuahidi kuzifanyia kazi.
Mbunge huyo amesema yupo kwaaajili ya kuwatumikia wananchi hivyo ni wajibu wake kusikiliza changamoto zao na kuzifanyia kazi hivyo wasiogope kumtuma kutekeleza majukumu mbalimbali ambayo yatailetea Ludewa Maendeleo.
“Nipo tayari kutumika kwaaajili ya Maendeleo ya wanaludewa hivyo nipo tayari kutumika na msiogope kueleza changamoto zenu kwa uwazi kabisa kwakuwa mimi ni mtumwa wenu na nipo hapa kwaajili ya kupokea maagizo kutoka kwenu”, Alisema Kamonga.
Sanjari na mkutano huo pia alitembelea shule ya sekondari Chief Kidulile ambapo alisikiliza changamoto mbalimbali kutoka kwa walimu pamoja nakupitia matokeo ya kidato cha nne ya mwaka 2018 na 2019 yalionekana kuto mfrahisha kwani kwa mwaka 2018 hakukuwa na division one yoyote, division two zilikuwa tano, division three nane, division four zikiwa 52 na mwaka 2019 nako hakukuwa na division one, two napo zilikuwa tano, division three 14 huku division four zikiwa 73.
Alisema matokeo hayo si mazuri hata kidogo kwani division four zimekuwa nyingi zaidi kitu ambacho hakileti picha nzuri hivyo amewaomba walimu kufundisha kwa bidii na endapo kutakuwa na changamoto inayohitaji utatuzi wake wasisite kumuambia ili kuondoa vikwazo vitakavyosababisha kushusha kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Ameongeza kuwa kuanzia sasa atakuwa ananunua kila alama ‘A’ itakayopatikana shuleni hapo ambapo atainunua kwa shilingi laki mbili ambayo ataikabidhi katika uongozi wa shule na mwalimu wa somo hilo atapata shilingi elfu hamsini.
“Nawaomba sana mfundishe kwa bidii ili kuinua kiwango cha ufaulu hapa shuleni, najua uwezo wenu wa kufundishia ni mzuri hivyo mimi mbunge wenu nipo tayari kutatua changamoto ambazo zinanihusu na zinaonekana kuwa kikwazo kwenu katika kufaulisha wanafunzi”, Alisema Kamonga.