Home Makala TBS ILIVYOFANIKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA KIPINDI CHA MIAKA 5 KATIKA SERIKALI...

TBS ILIVYOFANIKIWA KUTEKELEZA MAJUKUMU YAKE KWA KIPINDI CHA MIAKA 5 KATIKA SERIKALI YA AWAMU YA TANO

0

**************************

NA EMMANUEL MBATILO, 0673956262

Afya ya binadamu itakuwa njema kama atafuatilia kanuni na taratibu bora za afya, tunaishi kwa kutegemea afya bora pia afya bora inategemea na chakula ama bidhaa bora unayotumia ili iweze kukulinda.

Shirika la Viwango Tanzania TBS inawajibu kukuza viwango katika sekta ya viwanda na biashara kwa bidhaa zote zilizoagizwa na zilizoko viwandani katika kuingia soko la Tanzania. Mpango wa ukaguzi wa awali kwa usafirishaji wa bidhaa, unatumika kuratibu bidhaa zinazosafirishwa katika nchi husika, ili kuhakikisha bidhaa zote zingiizwazo zinaendana na taratibu za kiufundi zilizokubaliwa Tanzania, (viwango vilivyokubalika Tanzania au Kimataifa) kabla ya usafirishaji.

Hivyo jukumu kubwa la TBS ni kuhakikisha inalinda afya ya mlaji kwa kuhakikisha inadhibiti ubora wa bidhaa na vyakula kwa ujumla.

Serikali hutenga fedha kila mwaka kwa ajili ya kuhudumia wajasiriamali wadogo na wa kati pale wanapoomba bidhaa zao wanazozizalisha wenyewe zithibitishwe ubora. Katika utaratibu huu, wapo wajasiriamali ambao husamehewa kulipa ada yoyote kwa sababu ya mitaji yao kuwa midogo.

Mwaka 2019 Serikali ilipendekeza marekebisho ya sheria ya viwango sura 130 ili kuhamisha majukumu ya kusimamia masuala ya chakula na vipodozi kwa Shirika la Viwango Tanzania(Tanzania Bureau of Standards-TBS) kutoka Mamlaka ya Chakula na Dawa(Tanzania Food and Drugs Association-TFDA) ambapo baada ya sheria hiyo kupitishwa sasa TFDA imekuwa TMDA.

KUHUSU UTOAJI ELIMU YA UBORA WA BIDHAA

TBS imekuwa ikijitahidi kuzunguka katika mikoa mbalimbali kuwafikia wafanyabishara mbalimbali na kuweza kuwapatia elimu kuhusu umuhimu wa kutumia bidhaa zilizobora na zilizothibitishwa na Shirika hilo.

Muitikio wa utoaji wa elimu hiyo umekuwa ukizaa matunda kadri siku hadi siku kwa maana wengi wameshaanza kutambua umuhimu wa ubora wa bidhaa kuanzia wenye viwanda kwa maana wazalishaji pamoja na wafanyabiashara wadogo,wa kati na wakubwa.

TBS limekuwa likiwasisitiza wamiliki wa viwanda na bidhaa kuhakikisha wanapata alama ya ubora ili kuweza kuzalisha bidhaa iliyobora kumlinda mlaji na kuweza kukuza soko la bidhaa zinazozalishwa nchini.

Shirika hilo limekuwa likidhibiti kuingia kwa bidhaa ya chakula na vipodozi kwenye soko la Tanzania kama haijasajiliwa na shirika hilo.

Hivi karibuni Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt Athuman Ngenya, alikaririwa akisisitiza lazima majengo ya kuzalisha, kuhifadhi au kuuzia chakula, vipodozi pamoja na vyombo vinavyobeba bidhaa hizo ikiwemo magari ya kubebea nyama yawe yamesajiliwa na Shirika hilo, ndipo yataruhusiwa kutumika.

Mbali na hayo pia TBS imekuwa ikitoa elimu kwa waangizaji wa bidhaa na mawakala wa forodha nchini ili kuwawezesha wafanyabiashara kufanya biashara zenye tija kwa taifa bila kuathiri taratibu na sheria za nchi. 

UTOAJI WA MAFUNZO KATIKA KANDA

TBS limekuwa likitembelea kila kanda kutoa mafunzo bure kwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa bidhaa zinazozalishwa katika kanda hizo ili kuwahamasisha ni jisni gani wanaweza kuzalisha bidhaa zilizobora na kuweza kukuza uchumi wa nchi yetu kupitia bidhaa zinazozalishwa na viwanda vidogo na vikubwa katika nchi yetu.

TBS imekuwa ikitoa mafunzo hayo kwa kushirikiana na Wizara ya viwanda, SIDO, maafisa biashara, afya na maendeleo wa wilaya ili kuwajulisha wadau wa bidhaa kutumia fursa zilizopo ndani ya Serikali ili kuwawezesha kuboresha bidhaa zao ziweze kukidhi matakwa ya viwango na hatimaye kupananua wigo wa soko la ndani na nje ya nchi na kuwafanya kuongeza uzalishaji utakaopelekea kuinua uchumi wao.

Wazalishaji wamekuwa wakiaswa kuzingatia kanuni za uzalishaji na uhifadhi bora na salama ili kuepuka kupoteza masoko na kero ya kukutwa na bidhaa hafifu ambayo itawalazimu kuteketeza kwa gharama zao. 

MAFANIKIO KATIKA MAJUKUMU YAO

Katika kipindi cha miaka mitano ya Serikali ya Awamu ya Tano Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limefanikiwa kutekeleza mambo mbalimbali ili kuwezesha uwepo wa bidhaa safi zenye hadhi kwa matumizi ya wananchi.