……………………………………………………………..
Na.Alex Sonna,Dodoma
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mkoa na Serikali za Mitaa TAMISEMI Mhe. Selemani Jafo amewataka wakurugenzi wa Halmashauri tano (5) ambazo hazikufanya vizuri katika utekelezaji wa mkataba wa lishe kujieleza kwa Katibu Mkuu TAMISEMI ni kwanini hawakufikia malengo.
Maagizo hayo ameyatoa leo Jijini Dodoma wakati wa Mkutano wa tathmini ya nne mkataba wa lishe kwa mwaka wa fedha 2019 hadi 2020 ambapo amesema katika mkutano uliopita halmashauri therathini na tano (35) hazikufanya vizuri katika kutekeleza agizo la Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan na kuagiza wakatekeleze.
Ambapo licha ya maagizo hayo bado halmashauri tano (5) hazikutekeleza kikamilifu tena halmashauri hizo ni Chato, Bukoba, Misenye, Masasi na Bihalamuro hazikutekeleza na kufikia malengo yaliyowekwa.
“Mkajieleze kwa katibu Mkuu TAMISEMI ni kwanini hamkutekekeza mikataba ya hafua za lishe nimetaja halmashauri tano lakini hii ya Bihalamuro najua Mkurugenzi wake alibadilishwa huyu aliyepo akajieleze mikakati yake” amesema Waziri Jafo.
Licha ya kupongeza mikoa yote kwa kufanya vizuri lakini amesema kuna mikoa ya Kilimanjaro na Tabora haikufanya vizuri sana huku akiutaka Mkoa wa Rukwa kuongeza kasi kwani utekelezaji wake wa hafua za lishe haujafanya vizuri.
“Mkoa wa Rukwa licha ya kuwa katika Mikoa mitatu inayozalisha kwa wingi chakula lakini bado haijafanya vizuri katika kutekeleza mkataba wa hafua za lishe” amesema.
Aidha amesema bajeti ya lishe imekuwa ikiongezeka kadri siku zinavyoenda ambapo kwa 2018 hadi 2019 ilikuwa bilioni 15 lakini kwa sasa imepanda hadi kufikia 16.5 na utekelezaji kiasilimia umeongezeka kutoka asilimia 22 hadi kufikia asilimia 52.
Aidha amebainisha kuwa katika kuhamasisha jamii kuzingatia lishe bora wameanzisha siku ya lishe kitaifa ambapo itakuwa ikiadhimishwa kila tarehe 7 mwezi wa 8 kila mwaka pia kuanzisha mpango wa kugawa vyeti kwa halmashauri zinazofanya vizuri.
Amesema lishe bora ni muhimu hasa katika kipindi hiki ambapo tumeingia katika uchumi wa kati ili tujenge kizazi ambacho kitakuwa na afya bora na uwezo wa kufanya kazi kwa bidii.
Ametaja mikoa ambayo imefanya vizuri kuwa ni pamoja Kigoma iliyoshika nafasi ya kwanza, wa pili ni Arusha na watatu ni Mbeya, huku halmashauri zilizofanya vizuri ni Simanjiro, Iramba, Geita TC na Njombe DC.
Awali, Mkurugenzi wa Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe wa Ofisi hiyo, Dkt. Ntuli Kapologwe amesema malengo ya mkutano huo kuweka mikakati ili kuchunguza vikwazo vya lishe kwenye mikoa isiyofanya vizuri licha ya kuwa na uzalishaji mzuri wa chakula.