Home Mchanganyiko ALIYEKUWA MWENYEKITI WA RIVACU MIKONONI MWA TAKUKURU

ALIYEKUWA MWENYEKITI WA RIVACU MIKONONI MWA TAKUKURU

0

Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati.

*******************************************

Na Mwandishi wetu, Manyara
ALIYEKUWA Mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi wa chama cha ushirika cha Rift Valley Cooperative Union (RIVACU) Lohay Langay anashikiliwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa TAKUKURU kwa kutoa ajira bila idhini ya bodi ya wakurugenzi wa chama hicho.
Akizungumza na waandishi wa habari Mjini Babati, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Manyara, Holle Joseph Makungu amesema Langay anatuhumiwa kufanya kosa hilo Novemba mosi mwaka 2017 akiwa Mwenyekiti wa RIVACU.
Makungu amesema Langay akiwa Mwenyekiti wa RIVACU alitumia vibaya nafasi yake kwa kuingia mkataba wa ajira ya uhasibu kwa Paul Makoye bila idhini ya bodi ya wakurugenzi wa chama hicho cha ushirika.
“Katika uchunguzi wetu tumebaini kuwa katika mkataba huo Makoye aliingia mkataba bila idhini ya bodi ya wakurugenzi wa chama hicho cha ushirika na kujipatia ujira usio wa haki wa shilingi milioni 2.6,” amesema Makungu.
Amesema kitendo cha kuajiri bila kibali ni kosa la matumizi mabaya ya ofisi kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11 ya mwaka 2007.
“Langay anatarajiwa kufikishwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi wa mkoa wa Manyara na kusomewa shtaka hilo na mwendesha mashtaka wa TAKUKURU Wakili Martin Makani,” amesema Makungu.