Meneja wa NMB kanda ya Ziwa – Abraham Augustino akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini.
Afisa Mkuu wa Wateja Wadogo na Kati wa NMB Filbert Mponzi (kushoto) akimpa mkono Naibu Waziri wa Madini Stanslaus Nyongo baada ya kuzungumza na wachimbaji wadogo wa madini wa mkoa wa Geita, kwenye jukwaa la mtaji wa Maendeleo, katikati ni Mkuu Mkoa wa Geita- Robert Gabriel.
*********************
Geita. Wizara ya madini nchini imesema itaendelea kuzifuta leseni zote za utafiti ambazo hazifanyiwi kazi na zile ambazo hazilipiwi na kuwapatia wachimbaji wadogo hili waendelee kuzifanyia kazi ambazo zitasaidia kuinua uchumi wa nchi na kuzalisha ajira kwa vijana na watu ambao wanazunguka maeneo hayo.
Hayo yamesemwa Jana na Naibu waziri wa Madini Staslaus Nyongo wakati wa ufungaji wa Kongamano la Jukwaa la mitaji na maendeleo Mkoani Geita lililodhaminiwa na Benki ya NMB ambalo limefanyika kwa siku tatu kwenye ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Mji wa Geita.
Amesema Wizara imejidhatiti kuendelea kutoa maeneo ambayo yataongeza uzalishaji kwa wachimbaji wadogo na kwamba wanataka kuona wachimbaji wadogo wanainuka kiuchumi ili waweze kulipa mrabahaa wa serikali pamoja na kodi.
“Sisi kama wizara hatutakaa kimya kuona namna baadhi ya watu ambao wamekuwa wakipatiwa maeneo kwa ajili ya kufanya utafiti wanakaa nayo bila ya kuyashughulikia tutaendelea kuyataifisha maeneo hayo na kuwapa wachimbaji wadogo hili waweze kuinua vipato vyao”Alisema Naibu waziri Nyongo.
Aidha Waziri Nyongo aliishukuru Benki ya NMB kwa namna ambavyo imeendelea kuwa mstari wa mbele kuwasaidia wachimbaji wadogo ikiwa ni pamoja na kufadhili Kongamano hilo ambalo limedumu kwa siku tatu na kwamba anaamini elimu ambayo wameipata itawasaidia kuweka akiba na kujulikana shughuli ambazo wanazifanya ili iwe Rahisi kupatiwa Mikopo.
Mkuu wa Mkoa huo,Robert Gabriel alisema mkoa huo bado unakabiliwa na changamoto kubwa ya uhaba wa maeneo ya uchimbaji na kwamba ni vyema sasa kwa wizara kutuma wataalamu ambao wataweza kuja na kuona namna ambavyo watawasaidia kupata maeneo mengine ya uchimbaji.
Filbert Mponzi, ambaye ni afisa mkuu wa wateja wadogo na wakati NMB alisema Benki hiyo inatambua mchango wake mkubwa kwa jamii wakiwemo wachimbaji wadogo na ndio sababu ambayo imepelekea kufadhili semina hiyo ya siku tatu.
“Imani yetu ni kwamba maelekezo na elimu ambayo tumeitoa naamini wachimbaji wadogo wakiifanyia kazi sisi tupo tayari kuwakopesha tulikuwa tunashindwa kutokana na namna ambavyo walikuwa wakihama hama lakini naamini maelekezo tuliyowapa watayatekeleza”Alisema Filbert
Baadhi ya wachimbaji wadogo Mkoani humo,wameishukuru Benki ya NMB kuwa tayari kuwakopesha kwenye shughuli zao na kwamba kupitia mikopo ambayo watapatiwa itawasaidia kwa kiasi kuboresha shughuli zao za uchimbaji ambazo wamekuwa wakizifanya kila siku.