Mambo ni bandika – bandua, paukwa – pakawa ndani ya chaneli maarufu ya Maisha Magic Bongo (MMB) ambapo imetangaza rasmi kuanza kwa tamthilia mbili kabambe za Pazia na Jua Kali, zitakazoanza kurushwa kuanzia Januari 2021 kwenye Chaneli ya MMB DStv 160.
Kiu ya mashabiki wa tamthilia za kibongo imepata dawa kwani tamthilia mpya ya Pazia imepikwa ikapikika huku ikisimamiwa na mzalishaji maarufu na kijana mtanzania Samwel Isike, ambaye pia ndiye aliyezalisha tamthilia iliyojizolea umaarufu mkubwa hapa nchini ya Sarafu.
Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania Ronald Shelukindo akimtambulisha mzalishaji mkuu wa tamthilia mpya ya PAZIA Samwel Isike wakati wa uzinduzi rasmi wa tamthilia mpya za kitanzania za PAZIA na JUA KALI zinazorushwa katika chaneli ya Maisha Magic Bongo – DStv 160.
Tamthilia hii imeaanza kurushwa kuanzia January 4, 2021 na inaonekana Jumatatu hadi Jumatano saa 1:30 Jioni. Tamthilia hii imejaa mikasa, visa, vitimbi bila kusahau mafunzo yatokanayo na maudhui yake. Tamthilia hii imesheheni vinara wa uigizaji hapa nchini akiwemo Jacqueline Wolper anayeigiza kama Miriam Lewa bila kumsahau Hisani Muya anayeigiza kama Henry Lewa
Wasanii wanaoigiza katika tamthilia mpya ya PAZIA wakijitambulisha mbele ya waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa tamthilia mpya za kitanzania za PAZIA na JUA KALI zinazorushwa katika chaneli ya Maisha Magic Bongo – DStv 160. Miongoni mwa waigizaji hao ni (kutoka kulia) Tino Muya (Henry), Welu Sengo (Eliza), Ben Pol (Ben) Nasma Hassan (Regina) na Akim Juma (Edu).
Uhondo hauishii hapo, kwani mzigo mwingine unaoshushwa ndani ya MMB ni tamthilia ya Jua Kali kutoka kwa mzalishaji maarufu mwanadada Leah Mwendamseke, ambaye mbali ya kuwa ni mzalishaji wa tamthilia maarufu ya Kapuni pia ni mshindi wa tuzo mbalimbali katika tasnia ya filamu.
Wasanii wanaoigiza katika tamthilia mpya ya JUA KALI wakijitambulisha mbele ya waandishi wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa tamthilia mpya za kitanzania za PAZIA na JUA KALI zinazorushwa katika chaneli ya Maisha Magic Bongo – DStv 160. Miongoni mwa waigizaji hao ni – kutoka kushoto – Romy Jones (Bill Junior) Abbot Charles (Frank) Leah Mwendamseke na Wansukula Zacharia (Tuma).
Tamthilia hii ya Jua Kali itaanza kutingisha jiji mnamo Januari 6, 2021 na itakuwa ikirushwa saa 3.30 usiku Jumatano hadi Ijumaa. Huku nako kuna waigizaji nguli kama Rainfredd Masako anayeigiza kama Professor Bili na kumejaa vituko na mikasa ya kila aina ambapo wapenzi wa tamthilia hawatapenda kuikosa au kusubiri kusimuliwa.
Mtangazaji maarufu nchini Rainfred Masako ambaye anaigiza kama Profesa Bill katika tamthilia mpya ya JUA KALI akiwasalimu washiriki wa hafla ya uzinduzi rasmi wa tamthilia mpya za kitanzania za PAZIA na JUA KALI zinazorushwa katika chaneli ya Maisha Magic Bongo – DStv 160. Hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za DStv Tanzania ilihudhuriwa pia na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dr. Kiagho Kilonzo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa tamthilia hizo, Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dr. Kiagho Kilonzo, amesema kuwa serikali inathamini na kutambua mchango mkubwa wa MultiChoice katika kukuza na kuendeleza tasnia ya filamu hapa nchini. Amesema kitendo cha chaneli ya Maisha Magic Bongo kuwa na maudhui mengi ya ndani kimekuwa ni chachu ya ajira nyingi katika tasnia lakini pia kimeongeza ushindani na ubora wa kazi za wazalishaji wetu.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dr. Kiagho Kilonzo akizungumza wa habari wakati wa uzinduzi rasmi wa tamthilia mpya za kitanzania za PAZIA na JUA KALI zinazorushwa katika chaneli ya Maisha Magic Bongo – DStv 160. Hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za DStv Tanzania ilihudhuriwa pia nawasanii na waigizaji wa tamthilia hizo na waandishi wa habari.
Dr. Kiagho amesema kuwa yeye binafsi amekuwa akiwatemebelea wasanii na kujionea uzalishaji wa filamu mbalimbali hapa nchini na ameridhishwa na kuongezeka kwa ubora na weledi katika uzalishaji wa filamu na maudhui mengine. Amewataka wasanii kutumia fursa hii vizuri na kuhakikisha kuwa wanaongeza ubora wa kazi zao ili ziweze kushindana katika soko la ndani na nje na hivyo tasnia ya filamu kuongeza mchango wake katika uchumi wa wasanii na taifa kwa ujumla
Naye Mkuu Masoko wa MultiChoice Tanzania Ronald Shelukindo, amesema mbali na kutumia wasanii na waigizaji wakongwe, wamehakikisha kuwa kuna mchanganyiko na waigizaji wapya na vijana ambao wanaleta vionjo vipya na vya kisasa katika tamthilia hizo na hivyo kuzifanya kuwa kivutio kikubwa kwa watazamaji wa rika zote.
“Kila mara tunaleta maudhui kulingana na matakwa ya wateja wetu, tunhakikisha kuwa tunawapatia maudhui yaliyoboreshwa na yenye vionjo vipya kila uchao bila kusahau uhalisia wa kitanzania kwenye maudhui yetu” alisema Ronald na kuongeza kuwa wanafurahi sana kufanya kazi na wazalishaji na waigizaji wa Tanzania na hivyo kuzidi kukuza vipaji vya wasainii wetu na kuwapa ulingo wa kuonyesha umahiri wao katika fani.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Tanzania Dr. Kiagho Kilonzo (wa pili kulia) akiteta jambo na Mkuu wa Masoko wa MultiChoice Tanzania Ronald Shelukindo wakati wa uzinduzi rasmi wa tamthilia mpya za kitanzania za PAZIA na JUA KALI zinazorushwa katika chaneli ya Maisha Magic Bongo – DStv 160. Hafla hiyo iliyofanyika katika ofisi za DStv Tanzania ilihudhuriwa pia nawasanii na waigizaji wa tamthilia hizo.
Amesema kuwa katika miaka 5 tangu chaneli hiyo ianzishwe, mamia ya wazalishaji na wasanii wa Tanzania wamepata fursa ya kuuza kazi zao na hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa katika kukuza soko la maudhui hususan filamu hapa nchini.