Tanzania inaendelea kuimarisha ushirikiano na kampuni za kimataifa zinazobobea katika teknolojia za nishati ili kuongeza uzalishaji wa umeme, kuvutia mitaji na kukidhi mahitaji yanayoongezeka ya nishati nchini.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Balozi Dkt. Mahmoud Thabit Kombo (Mb.), ameongoza ujumbe wa Tanzania katika mazungumzo na Kampuni ya Siemens Energy katika kiwanda cha kampuni hiyo kilichopo Finspång, Sweden.
Mazungumzo hayo yamejikita kuangazia ushirikiano katika utekelezaji wa miradi ya uzalishaji wa umeme kwa kutumia gesi asilia, kuimarisha ubia kati ya sekta ya umma na sekta binafsi, pamoja na kuvutia uwekezaji na mitaji kutoka taasisi za fedha za kimataifa.
Siemens Energy imepongeza mkakati wa Tanzania wa kuongeza mitambo ya kuzalisha umeme itakayowezesha kuongeza upatikanaji umeme nchini pamoja na kubidhaisha umeme wa Tanzania. Hatua hiyo inaongeza imani ya wawekezaji na kuharakisha utekelezaji wa miradi.
Aidha, Mchambuzi wa Fedha Mwandamizi kutoka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Bi. Elizabeth Soud Ally ameeleza utayari wa shirika hilo katika kuwezesha uwekezaji wa sekta binafsi katika uzalishaji wa umeme kupitia mikataba ya ununuzi wa umeme na uunganishaji wa miradi katika gridi ya taifa.
Mhe. Kombo pia amepata fursa ya kutembelea kiwanda hicho kujionea teknolojia za kisasa za utengenezaji wa mitambo ya kuzalisha umeme, pamoja na fursa za uhawilishaji wa teknolojia na ukuzaji wa ujuzi kwa wataalamu wa Tanzania.

