Na Mwandishi wetu, Simanjiro 

WAKAZI wa Kijiji cha Naisinyai Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wameipongeza kampuni ya Franone Mining & Gems LTD kwa kuwanunulia tenki la kuhifadhia maji lenye ujazo wa lita 10,000 na kuwapatia tawi la maji wanayonyweshea mifugo na jamii ya eneo la Samax kupatiwa vilula viwili vya maji.

Mwenyekiti wa kijiji cha Naisinyai, Joseph Maliaki Laizer ameishukuru kampuni ya Franone Mining & Gem LTD kwa kuwezesha tenki hilo la maji na mifugo kuandaliwa eneo la kunyweshea maji na jamii ya eneo la Samax kupata maji.

“Tunamshukuru Mkurugenzi wa kampuni ya Franone Mining & Gem LTD Onesmo Mbise kwa kutupatia tenki hilo na maji hayo ambayo wafugaji wanayatumia kunyweshea mifugo na jamii inatumia bila kulipia fedha yoyote,” amesema Mwenyekiti Maliaki.

Mwenyekiti wa jumuiya ya umoja wa vijana (UVCCM) Kata ya Naisinyai, Patimayo Mollel akisoma taarifa amesema wananchi wa eneo hilo wanatoa shukran zao za dhati kwa kampuni hiyo kwa kuwezesha huduma hiyo ya maji.

“Tunaishukuru kampuni ya Franone kwa kutupatia tawi la maji linalotumika kunyweshea mifugo na vitalu viwili vya maji katika eneo la Samax kwa ajili ya wananchi wanaoishi eneo hilo,” amesema Mollel.

Diwani wa Kata ya Naisinyai Taiko Kurian Laizer ameishukuru kampuni ya Franone Mining & Gem LTD kwa misaada hiyo ambayo inanufaisha jamii ya eneo hilo.

“Kila mara Franone Mining & Gem LTD mmekuwa mstari wa mbele wa kuwezesha CSR kwa jamii inayowazunguka hivyo wachimbaji wengine waige mfano wenu,” amesema Diwani Taiko.

Hata hivyo, meneja wa mgodi wa kampuni ya Franone Mining & Gem LTD Frank Mziwanda ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa kampuni hiyo Onesmo Mbise amesema atafikisha salamu zao za shukrani kwa uongozi wa kampuni hiyo.

Mziwanda amesema gharama za tenki hilo la maji lenye uwezo wa kuhifadhi lita 10,000 za maji lina thamani ya 3,000,000 lililonunuliwa na kampuni ya Franone Mining & Gem LTD.

“Mkurugenzi wa kampuni amenieleza niwaambie kuwa milango ya kampuni ipo wazi endapo kuna jambo la kufikisha kwa uongozi mnakaribishwa,” amesema Mziwanda.