Na Silivia Amandius, Kagera.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Bukoba, Proscovia Jaka Mwambi, amelitaka Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wazazi na jamii kuongeza juhudi za kuwalinda watoto, hususan watoto wa kike, dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia ili kukomesha matukio hayo yanayoendelea kuripotiwa katika Wilaya ya Bukoba.

Mwambi ametoa wito huo leo wakati wa uzinduzi wa kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia kimkoa, uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Kashai, Manispaa ya Bukoba, akiwa mgeni rasmi kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera. Amesisitiza kuwa mapambano dhidi ya ukatili yanahitaji ushirikiano wa familia, jamii, taasisi za serikali na wadau mbalimbali ili kulinda haki na usalama wa wanawake na watoto.

Awali, Mkuu wa Kitengo cha Polisi Jamii Mkoa wa Kagera, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Charles Mimata, amesema Wilaya ya Bukoba imeongoza kwa kuripotiwa kwa makosa ya ukatili wa kijinsia na watoto mkoani humo, baada ya kurekodi matukio 60 katika kipindi cha Januari hadi Novemba 2026.

Amesema kati ya matukio hayo, 51 ni ubakaji, sita ulawiti, mauaji ya mtoto mmoja na mauaji ya wanawake wawili. Ameeleza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea kushirikiana na taasisi za serikali na zisizo za serikali kutoa elimu kwa jamii, huku katika kipindi hicho mikutano zaidi ya 960 ikifanyika kupitia wakaguzi wa kata kwa lengo la kuelimisha wananchi, hususan wanafunzi, kuhusu namna ya kujikinga na kuripoti vitendo vya ukatili.

Aidha, ACP Mimata amesema Jeshi la Polisi limeimarisha Dawati la Jinsia na Watoto pamoja na huduma ya kupokea taarifa kupitia namba 0699 913 200 inayopatikana saa 24 bila malipo. Ameongeza kuwa takwimu zinaonesha ubakaji umepungua kutoka matukio 221 mwaka 2025 hadi 205 mwaka 2026, wakati ulawiti umeongezeka kutoka 12 hadi 16 na mauaji ya watoto kutoka tisa hadi 10. Mauaji ya wanawake yamepungua kutoka 42 hadi 19 katika kipindi hicho.

Uzinduzi huo ni sehemu ya kampeni ya siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, iliyoanza kitaifa Novemba 25 mwaka huu mkoani Dodoma, ikiwa na lengo la kuhamasisha jamii kutambua, kuzuia na kutoa taarifa za vitendo vya ukatili, pamoja na kujenga jamii salama inayoheshimu haki za wanawake na watoto.