Na.sophia Kingimali.
Baraza la Watumiaji Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC) limewaonya wananchi kuhusu vitendo vya utapeli vinavyofanywa na baadhi ya watu katika vituo vya mabasi, likiwataka kutumia mifumo rasmi ya kielektroniki kukata tiketi za safari zao kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Akizungumza katika maonesho ya maadhimisho ya Siku ya Usafiri Endelevu Duniani jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa LATRA CCC, Daudi Daudi, amesema matumizi ya tiketi za kielektroniki yatasaidia kupunguza udanganyifu na kulinda fedha za abiria dhidi ya watu wanaouza tiketi zisizo na uthibitisho.
Amesema baadhi ya watu wamekuwa wakijitokeza katika vituo vya mabasi, hususan stendi, wakijifanya kuwa na uwezo wa kuwasaidia abiria kupata tiketi, hali inayoweza kusababisha wananchi kulipia huduma ambazo hawana uhakika nazo.
Daudi amesema abiria hawana ulazima wa kufika katika vituo vya mabasi ili kupata tiketi, kwa kuwa wanaweza kukata wakiwa nyumbani au mahali popote walipo kwa kutumia simu janja, kompyuta mpakato au kifaa kingine chenye huduma ya intaneti.
Amesema wananchi wanaweza kupata huduma hiyo kwa kupitia tovuti ya Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA), www.latra.go.tz, na kufuata kiunganishi kinachowaelekeza kwenye mfumo wa tiketi za kielektroniki unaounganisha watoa huduma mbalimbali za usafiri.
Ameongeza kuwa mfumo huo umeunganisha huduma za ukataji tiketi za mabasi na reli, hatua inayomwezesha mwananchi kupata huduma kupitia sehemu moja bila kulazimika kutafuta mifumo tofauti kwa kila kampuni ya usafiri.
Akizungumzia maandalizi ya safari za Desemba, Daudi amewataka abiria na watoa huduma kupanga safari zao mapema kutokana na ongezeko la mahitaji ya usafiri katika kipindi cha sikukuu, huku akisisitiza umuhimu wa wananchi kufahamu haki na wajibu wao.
Amesema LATRA CCC imeshiriki maadhimisho hayo yanayofanyika Novemba 26 kila mwaka kwa lengo la kutoa elimu kwa wananchi kuhusu huduma za usafiri, ambapo katika siku tatu za maonesho hayo banda la baraza lilipokea takribani watu 200 waliopata elimu mbalimbali.
Amesema baraza hilo linaendelea na mikakati ya kuwafikia wananchi katika mikoa yote ya Tanzania Bara kupitia kamati za watumiaji huduma za usafiri za mikoa, vyombo vya habari na majukwaa ya kidijitali ili kuongeza uelewa kuhusu matumizi sahihi ya huduma hizo.
Naye Mkuu wa Idara ya Fedha na Utawala wa LATRA CCC, Fatuma Kulita, amewahimiza wananchi kukata tiketi za safari zao mapema kupitia mifumo ya mtandao ili kuepuka usumbufu na changamoto za utapeli zinazoweza kujitokeza wakati wa kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Amesema baraza hilo limekuwa likitoa elimu kuhusu haki na wajibu wa watumiaji wa huduma za usafiri ardhini, akisisitiza kuwa matumizi ya mifumo rasmi ya mtandao katika ununuzi wa tiketi ni hatua muhimu ya kujilinda dhidi ya matapeli na kuhakikisha abiria wanapata huduma kwa utaratibu unaostahili.

