Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

RAIS Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema dhamana aliyopewa ya kuwa Kinara wa Umoja wa Afrika (AU) wa Afya ya Mama na Mtoto itatumika kuharakisha utekelezaji wa mikakati ya kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa wanawake na watoto katika bara hilo ifikapo mwaka 2030.

Amesema mpango elekezi wa mwaka 2026 hadi 2030 aliouzindua unalenga kuunganisha uongozi wa kisiasa, uwekezaji na uwajibikaji wa nchi wanachama ili kuhakikisha ajenda ya afya ya mama na mtoto inatekelezwa kwa vitendo na kuleta matokeo yanayopimika.

Akizungumza leo Novemba 26,2026 jijini Dar es Salaam wakati wa kufungua Mkutano wa Tatu wa Kisayansi wa Afya ya Uzazi, Mama, Mtoto Mchanga, Mtoto, Vijana na Lishe (RMNCAH+N), alisema mafanikio ya Tanzania katika kupunguza vifo vya mama na watoto yanaweza kuwa mfano kwa mataifa mengine ya Afrika.

Amesema mpango huo umejengwa katika dhana ya Sufuri Tatu, ikiwemo kuhakikisha hakuna mwanamke anayejifungua nje ya kituo cha afya, hakuna kifo cha mama au mtoto kinachoweza kuzuilika na hakuna mtoto anayekosa chanjo.

Rais Samia amesema dhamana hiyo haitapimwa kwa idadi ya mikutano au mipango inayowekwa, bali kwa matokeo yatakayopatikana katika kuokoa maisha, kuimarisha mifumo ya afya na kuongeza uwajibikaji wa viongozi wa nchi za Afrika.

Amesema mfumo wa tathmini na ufuatiliaji uliowekwa utasaidia nchi wanachama kupima maendeleo, kubaini changamoto zinazokwamisha utekelezaji na kufanya maamuzi ya haraka ili kuhakikisha malengo yaliyowekwa yanafikiwa.

Amewataka wakuu wa mikoa kusimamia mikataba waliyoingia na Serikali kuhusu kuboresha huduma za afya ya uzazi, mama, mtoto na vijana, huku Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais-TAMISEMI zikihakikisha utekelezaji wake unafuatiliwa kwa karibu.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, wadau wa maendeleo, sekta binafsi, taasisi zisizo za kiserikali na madhehebu ya dini katika kuimarisha huduma za afya na kuongeza uwekezaji kwenye lishe bora kwa wajawazito na watoto.

Amesema matarajio yake ni kuona dhamana hiyo ikisaidia viongozi wa Afrika kuweka vipaumbele vinavyotekelezeka, kuimarisha uwajibikaji, kuunganisha ufadhili na kuharakisha juhudi za kutokomeza vifo vinavyoweza kuzuilika kwa wanawake na watoto.