Na Farida Mangube Morogoro
Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) imeendelea kuimarisha uwezo wake wa kiutendaji kwa kuongeza vitendea kazi, ikiwemo magari, ili kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa mbegu mashambani na katika maduka ya pembejeo, pamoja na kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora na sahihi kwa ajili ya uzalishaji.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kukabidhiwa gari mapya yaliyotolewa kwa ajili ya kuimarisha shughuli za taasisi katika maeneo kanda ya ziwa , Mkurugenzi Mkuu wa TOSCI, Nyasebwa Chimagu, amesema taasisi hiyo imejipanga kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika usimamizi wa ubora wa mbegu, huku ikiendelea kutoa elimu kwa wakulima kuhusu matumizi ya mbegu bora na sahihi.
Amesema upatikanaji wa vitendea kazi ikiwemo magari ni hatua muhimu katika kuongeza nguvu ya ukaguzi wa mbegu katika maeneo ya uzalishaji na kwenye maduka ya pembejeo, ili kuhakikisha mbegu zinazouzwa na kutumika na wakulima zinakidhi viwango vya ubora vinavyotakiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya TOSCI, Lilian Schechambo, amesema mpaka sasa magari 18 yamekabidhiwa kwa taasisi ikiwemo mengine yamenunuliwa kwa kutumia fedha za ndani za taasisi, hatua inayoonesha dhamira ya kuendelea kuboresha huduma na kuimarisha usimamizi wa upatikanaji wa mbegu bora nchini.
Naye Mkuu wa Kanda ya Ziwa wa TOSCI, Ayubu Mshema, amesema kanda hiyo imepokea magari matatu ambayo yataongeza ufanisi wa shughuli za ukaguzi, usimamizi na utoaji wa elimu kwa wadau wa sekta ya mbegu, hivyo kuimarisha huduma kwa wakulima katika maeneo ya kanda hiyo.

