
Serikali ya Tanzania na Shirika la Maendeleo la Ufaransa (AFD) zimesaini mikataba mitatu ya mikopo yenye masharti nafuu yenye thamani ya euro milioni 175 sawa na takriban shilingi bilioni 513), kwa ajili ya kutekeleza miradi ya huduma za maji na usafi wa mazingira katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria, miundombinu ya chakula Mwanza na Tanga, na maendeleo ya uvuvi pamoja na wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa.Mikataba hiyo imesainiwa na Waziri wa Fedha, Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa AFD, Bw. Christophe Lecourtier, tukio lililofanyika Makao Makuu ya AFD jijini Paris, kando ya Jukwaa la 25 la la Kimataifa la Uchumi Afrika-OECD.Kusainiwa kwa mikataba hiyo, kunafanya jumla ya thamani ya ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na AFD kufikia euro bilioni 1.3 sawa na takriban shilingi trilioni 3.81 ambapo fedha hizo zimetumika kutekeleza miradi mbalimbali ya kiuchumi na kijamii kwenye huduma na shughuli zinazogusa maisha ya wananchi moja kwa moja zikiwemo sekta za maji, kilimo, nishati na ujenzi wa miundombinu.Mkataba wenye thamani kubwa zaidi, wa euro milioni 90 (Sh bilioni 263.8), unafadhili Awamu ya Pili ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika maeneo yanayozunguka Ziwa Victoria, ukilenga kuboresha upatikanaji wa maji na huduma za usafi wa mazingira kwa wakazi wa maeneo hayo.
Mkataba wa pili, wa euro milioni 55 (Sh bilioni 161.2), unafadhili Programu ya Uwekezaji Endelevu katika Mifumo ya Chakula Mijini (TASUFIP). Programu hiyo inalenga kuboresha miundombinu inayohudumia biashara na usambazaji wa chakula katika miji ya Mwanza na Tanga.
Mkataba wa tatu, wa euro milioni 30 (Sh bilioni 87.9), unafadhili Programu ya Kuendeleza sekta ya uvuvi na Ufugaji wa Ng’ombe wa Maziwa kwa Wafugaji Wadogo kwa Kuzingatia Mabadiliko ya Tabianchi nchi nzima.
Programu hiyo, inayofadhiliwa kwa pamoja na Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), pamoja na wadau wengine ambao ni OPEC Fund, na Green Climate Fund, inalenga kuimarisha uzalishaji wa mazao ya uvuvi, maziwa na kuimarisha uwezo wa wafugaji wadogo kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Waziri wa Fedha Mhe Balozi Khamis alieleza kuwa maana ya saini hizo itaonekana katika utekelezaji wa miradi yenyewe, ikiwa ni hatua zinazochukuliwa na Serikali kuboresha huduma na maisha ya wananchi.
“Kwa familia zinazoishi kandokando ya Ziwa Victoria, ni huduma bora za maji na usafi wa mazingira, kwa wafanyabiashara wa chakula Mwanza na Tanga, ni miundombinu bora ya kufanyia biashara. Kwa wavuvi na wafugaji wadogo wa ng’ombe wa maziwa, ni uwezo wa kuendeleza uzalishaji licha ya athari za mabadiliko ya tabianchi” alisema Mhe. Balozi Omar
Mhe. Balozi Khamis Mussa Omar aliishukuru Ufaransa, kupitia AFD, kwa ushirikiano wa muda mrefu na msaada unaoendelea kwa vipaumbele vya maendeleo ya Tanzania, akieleza kuwa ushirikiano huo umejengwa juu ya kuaminiana kwa pande zote, malengo ya pamoja ya maendeleo na dhamira ya kuinua maisha ya wananchi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Maendeleo la Ufaransa AFD, Bwana Christophe Lecourtier, alisema kuwa Ufaransa kupitia Shirika lake linathamini ushirikiano wa kimaendeleo wa muda mrefu na Tanzania na kwamba wako tayari kuendeleza ushirikiano huo kwa faida ya pande zote mbili.
Ameeleza kuwa Shirika lake linaangalia maeneo mengine ya ushirikiano na Tanzania katika kutekeleza miradi yake ya kimkakati itakayochochea ukuaji wa Uchumi na maisha ya wananchi kwa ujumla
Kikao hicho kilihudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mheshimiwa Saidi Othman Yakubu, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Asha Khamis Abdulla, na Kamishna wa Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. Rished Bade.
