Na. Meleka Kulwa- Fullshangwe Blog,Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki maadhimisho ya Siku ya UKIMWI Duniani yanayotarajiwa kufanyika Desemba Mosi, 2026, jijini Dodoma.
Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 26, 2026, jijini Dodoma, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuwakumbuka watu waliopoteza maisha kutokana na UKIMWI, kutathmini mafanikio na changamoto zilizopo katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Amesema kuwa maadhimisho hayo yanafanyika kuanzia Novemba 24 hadi Desemba Mosi, 2026, katika Ukumbi wa Jakaya, yakiratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania.
Aidha, amebainisha kuwa maadhimisho hayo yatakuwa na maonyesho ya wadau mbalimbali wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya UKIMWI nchini, pamoja na utoaji wa elimu na huduma zinazohusiana na VVU na UKIMWI.
Pia, amesema kuwa kutakuwa na hamasa ya upimaji wa hiari wa VVU, ikiwemo huduma za kujipima mwenyewe, ili kuwawezesha wananchi kufahamu hali zao za kiafya na kuchukua hatua stahiki.
Ameongeza kuwa kutakuwa na afua maalumu za utoaji wa elimu kuhusu VVU na UKIMWI kwa makundi yaliyo katika hatari zaidi ya kupata maambukizi, hususan vijana.
Pia, amesema kuwa wananchi watakaohudhuria maadhimisho hayo watanufaika na huduma mbalimbali za kiafya, ikiwemo upimaji wa VVU, saratani, kisukari pamoja na upimaji wa uwiano wa urefu na uzito.
Aidha, amebainisha kuwa taasisi za RITA na NIDA pamoja na watoa huduma za msaada wa kisheria zitashiriki katika maadhimisho hayo kwa kutoa huduma na elimu mbalimbali kwa wananchi.
Amesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yanabeba kaulimbiu isemayo “Huduma Bora za Afya ni Msingi wa Kutokomeza UKIMWI,” inayosisitiza umuhimu wa upatikanaji wa huduma bora za afya katika kuimarisha mapambano dhidi ya UKIMWI.
Katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, huku wananchi wakihimizwa kujitokeza kushiriki shughuli mbalimbali zitakazofanyika.

