Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

TANZANIA inatarajia kutumia mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 kujitangaza kimataifa kupitia utalii, utamaduni na fursa za biashara, huku ikilenga kuongeza idadi ya wageni na kuimarisha nafasi yake katika ramani ya kimataifa.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, amesema mashindano hayo yatakayofanyika kwa ushirikiano wa Tanzania, Kenya na Uganda ni fursa ya kihistoria kwa Afrika Mashariki kuonyesha uwezo wake wa kuandaa matukio makubwa ya kimataifa.

Makonda amesema Tanzania inapaswa kutumia mwanya huo kuonyesha vivutio vyake vya utalii, utamaduni na maendeleo yaliyofikiwa, ili wageni watakaofika nchini wakati wa mashindano hayo wawe mabalozi wa kuitangaza nchi katika mataifa yao.

Amesema mashindano hayo yanatarajiwa kushirikisha timu 24 zitakazocheza mechi 52 kwa siku 29, huku Tanzania ikitarajiwa kuwa mwenyeji wa sehemu kubwa ya michezo hiyo katika miji ya Dar es Salaam, Arusha na Zanzibar.

Amesema maandalizi ya mashindano hayo yanafanyika kwa ushirikiano wa viongozi wa nchi hizo tatu, akiwapongeza Rais wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Uganda, Yoweri Museveni na Rais wa Kenya, William Ruto kwa kuunganisha nguvu kuhakikisha tukio hilo linafanikiwa.

Aidha, amesema matumizi ya lugha ya Kiswahili kama lugha rasmi ya mashindano hayo yanatarajiwa kuongeza hadhi ya lugha hiyo kimataifa na kutoa nafasi kwa utamaduni wa Afrika Mashariki kutambulika zaidi duniani.

Makonda amesema Tanzania inajiandaa kupokea timu, viongozi, mashabiki na wageni kutoka mataifa mbalimbali kwa kuhakikisha kunakuwepo huduma bora za malazi, usafiri na mazingira rafiki kwa wageni watakaotembelea nchi hiyo.

Ameeleza kuwa ongezeko la wageni linatarajiwa kuongeza mahitaji ya huduma za hoteli, usafiri, utalii na biashara mbalimbali, hivyo kuwataka wafanyabiashara kujiandaa mapema kwa kuboresha huduma, kusajili biashara zao na kutumia mitandao ya kijamii kutangaza bidhaa na huduma wanazotoa.

Pia amewahimiza wananchi kujifunza lugha za kimataifa ikiwemo Kiingereza, Kifaransa na Kiarabu ili kurahisisha mawasiliano na wageni, akisisitiza kuwa maandalizi ya AFCON 2027 yanapaswa kuwashirikisha wananchi katika nyanja mbalimbali badala ya kuishia kwenye viwanja na miundombinu pekee.

Makonda amesema mafanikio ya mashindano hayo hayatapimwa kwa ubora wa viwanja au matokeo ya michezo pekee, bali pia kwa namna Tanzania itakavyoweza kujitangaza, kuvutia watalii, kukuza biashara na kuimarisha ushirikiano na mataifa mengine.

Amempongeza Rais Samia kwa uwekezaji na msukumo alioutoa katika maandalizi ya mashindano hayo, akisema Watanzania wana wajibu wa kutumia fursa hiyo kukuza uchumi na kujenga taswira nzuri ya nchi kimataifa