NA DENIS MLOWE IRINGA
MKUU wa Wilaya ya Mufindi, Dkt. Linda Salekwa, ameongoza Madiwani na wataalamu wa Halmashauri ya Mji Mafinga katika ziara ya mafunzo ya kimkakati inayolenga kujifunza namna ya kuwekeza na kuendeleza viwanja vya michezo ili kukuza vipaji, kuongeza mapato ya halmashauri na kuboresha huduma za burudani kwa wananchi.
Ziara hiyo iliyofanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Arusha, imehusisha Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji Mafinga, Regnant Kivinge, pamoja na wataalamu wa halmashauri hiyo wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi, Peter Ngussa, ambapo wamejifunza mifumo ya uwekezaji na usimamizi wa miundombinu ya michezo.
Halmashauri ya Mji Mafinga imeeleza kuwa tayari imetenga eneo kwa ajili ya uwekezaji wa viwanja vya michezo, mradi unaotarajiwa kuwa na mchango mkubwa katika kuibua na kukuza vipaji vya michezo kwa wakazi wa mji huo, kuongeza mapato ya halmashauri na kutoa nafasi za mapumziko na burudani kwa wananchi pamoja na wageni.
Katika ziara hiyo, ujumbe huo umetembelea kituo cha FUTURE STARS (Youth Empowerment Centre), kinachojihusisha na kukuza vipaji vya mpira wa miguu, ambacho kinafanya kazi kwa mfumo wa ubia kati ya Halmashauri na mwekezaji, hatua iliyowapa fursa ya kujifunza namna ya kushirikisha sekta binafsi katika kuendeleza miundombinu na programu za michezo.
Aidha, ujumbe huo umetembelea Tanzanite Kwarra Stadium iliyopo Babati, Arusha, ambako wamepata maelezo kuhusu umiliki wa eneo hilo, hatua zilizofuatwa na taratibu za ujenzi na uendelezaji wa uwanja huo, ikiwa ni sehemu ya kujifunza mbinu zinazoweza kutumika katika kutekeleza mradi wa viwanja vya michezo Mafinga.
Uwekezaji huo unatarajiwa kuwa chachu ya maendeleo ya michezo katika Mji wa Mafinga, huku ukiwa na nafasi ya kuimarisha uchumi wa halmashauri kupitia shughuli za michezo, mashindano, burudani na huduma mbalimbali zitakazozunguka miundombinu hiyo.

