Naibu Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Watu wa Ethiopia, Mhe. Temesgen Tiruneh, amefungua rasmi Mkutano wa Jukwaa la Maendeleo ya Biashara Afrika jijini Addis Ababa, Ethiopia, wenye lengo la kujadili fursa za biashara kwa nchi za Afrika na namna zinavyoweza kutumia soko la Afrika kuuza bidhaa zao.

Mkutano huo pia unajadili changamoto mbalimbali zinazosababisha nchi za Afrika kushindwa kutumia kikamilifu fursa za masoko ya bara hilo na namna ya kuzitatua kwa pamoja.

Akizungumza katika ufunguzi wa mkutano huo, Mhe. Tiruneh amesema nchi nyingi za Afrika zina bidhaa nyingi na uwezo wa kuzalisha kwa ajili ya kuuza, lakini changamoto kubwa ni kuuza bidhaa ambazo hazijachakatwa, hali inayozikosesha mapato yanayostahili.

Amewataka Mawaziri wa Afrika wanaoshiriki jukwaa hilo kuhakikisha wanahamasisha uuzaji wa bidhaa zilizoongezwa thamani kupitia uchakataji, ili kuongeza mnyororo wa thamani na kutumia ipasavyo fursa zinazotolewa na soko la Afrika.

Mkutano huo wa Jukwaa la Maendeleo ya Biashara Afrika umeandaliwa na Serikali ya Ethiopia kwa kushirikiana na Trademark Africa, ukishirikisha Mawaziri wa Viwanda, Biashara na Utangamano wa Kibiashara kutoka nchi mbalimbali za Afrika pamoja na wadau wa uwekezaji kutoka nje ya bara hilo.

Lengo la mkutano huo ni kujadili fursa za uwekezaji barani Afrika, changamoto zinazokwamisha biashara na kuweka mikakati ya pamoja ya kuzitatua.

Sambamba na mkutano huo, pia imezinduliwa Ripoti ya Maendeleo ya Biashara kwa Nchi za Afrika ya mwaka 2026.

Tanzania inashiriki katika mkutano huo kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, ambapo Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, anaongoza ujumbe wa Tanzania unaojumuisha taasisi za TanTrade na TBS, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Dkt. Natu Mwamba, Ubalozi wa Tanzania nchini Ethiopia, wadau wa sekta binafsi pamoja na wafanyabiashara.