Berlin, Ujerumani

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Shirikisho la Ujerumani zimehitimisha majadiliano ya ushirikiano wa maendeleo kwa kusaini Hati ya Makubaliano itakayoongoza ushirikiano wa nchi hizo mbili katika miaka ijayo.

Majadiliano hayo yamefanyika tarehe 18 na 19 Novemba 2026, jijini Berlin, Ujerumani.

Hati hiyo imesainiwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, Bi. Asha Khamis Abdulla, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania, na Bi. Christine Toetzke, Mkurugenzi Mkuu anayeshughulikia Ushirikiano wa nchi hizo mbili katika Wizara ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo (BMZ), kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani.

Katika majadiliano hayo, nchi hizo mbili zimejadili kuimarisha ushirikiano katika sekta za maji, nishati, usimamizi bora wa fedha za umma, mageuzi ya kidijitali, upatikanaji wa haki, afya, huduma za kijamii na uhifadhi wa mazingira.

Aidha, Ujerumani imeahidi kuipatia Tanzania ufadhili mpya wa hadi Euro milioni 116 kupitia mikopo yenye riba nafuu katika kioindi cha miaka miwili ijayo (2037-2028) kwa ajili ya miradi ya maji, nishati na ambapo kati ya fedha hizo, hadi Euro milioni 50 zimependekezwa kutumika kwa ajili ya Mradi wa Maji na Usafi wa Mazingira katika Ziwa Victoria, Awamu ya Tatu (LVWATSAN III), mkoani Mwanza.

Kiasi kingine cha hadi Euro milioni 50 kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya umeme, ikiwemo ukarabati wa Kituo cha Kufua Umeme cha Kidatu na upanuzi wa Kituo cha Umeme cha Ifakara, mkoani Morogoro.

Vilevile, majadiliano hayo yamehusisha ufadhili wa kitaalamu wa euro milioni 16 katika maeneo ya usimamizi wa fedha za umma, mageuzi ya kidijitali, uimarishaji wa huduma za maji Tanzania Bara na Zanzibar, pamoja na upatikanaji wa haki kwa wanawake na watoto.

Akizungumza katika majadiliano hayo kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Dkt. Natu El-Maanry Mwamba, Naibu Katibu Mkuu, Wizara ya Fedha, Bi. Asha Khamis Abdulla amesisitiza umuhimu wa kuhakikisha ushirikiano huo unaendana na Dira 2050, na Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (FYDP IV), unazingatia vipaumbele vya Serikali na unachangia ukuaji wa uchumi, uboreshaji wa huduma za kijamii na ustawi wa wananchi.

Pia, amesisitiza umuhimu wa matumizi yenye tija ya rasilimali, usimamizi endelevu wa deni la umma, maandalizi bora ya miradi na kuimarisha uratibu wa utekelezaji wa miradi inayofadhiliwa na washirika wa maendeleo.

Kwa upande wake kiongozi wa ujumbe wa Ujerumani Bi. Kofler alisema, Tanzania ni mshirika wa kuaminika na kwamba Ujerumani inatoa ahadi zake za kufadhili utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kiuchumi kulingana na vipaumbele vya Tanzania kwa manufaa ya wananchi wake.

Utiaji saini wa Hati hiyo ni hatua muhimu katika kuendeleza ushirikiano wa maendeleo kati ya Tanzania na Ujerumani uliodumu kwa zaidi ya miaka 60, ambapo nchi hizo mbili zimeendelea kushirikiana katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Serikali ya Tanzania imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuimarisha ushirikiano na Serikali ya Ujerumani ili kuharakisha utekelezaji wa miradi ya kimkakati na kufanikisha malengo ya maendeleo ya Taifa.