Na Sophia Kingimali, Dar es Salaam

SERIKALI inatarajia kutumia maadhimisho ya mwaka mmoja wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana kuwasilisha mafanikio yaliyopatikana katika sekta hiyo, kueleza programu zinazotekelezwa na kuweka bayana vipaumbele vya kuwawezesha vijana katika kipindi kijacho.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Novemba 21,2026 Jijini Dar es salaam Waziri wa Maendeleo ya Vijana, Joel Nanauka, amesema maadhimisho hayo yanalenga kuongeza uelewa wa umma kuhusu majukumu ya ofisi hiyo, matokeo ya utekelezaji wa programu zake na namna Serikali inavyoshirikiana na wadau kufungua fursa kwa vijana.

Amesema tukio hilo litawakutanisha taasisi za Serikali, sekta binafsi, asasi za kiraia, wadau wa maendeleo na vijana wenyewe kwa ajili ya kutathmini mafanikio yaliyopatikana katika mwaka mmoja na kujadili mwelekeo wa maendeleo ya vijana nchini.

Nanauka amesema katika maadhimisho hayo, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajiwa kuzindua Mfumo wa Uwezeshaji wa Vijana (Youth Empowerment System – YES) pamoja na Mfumo wa Uratibu wa Maendeleo ya Vijana.

Amesema mfumo wa YES utarahisisha upatikanaji wa taarifa za fursa na huduma zinazotolewa na Serikali pamoja na wadau mbalimbali, huku ukiwaunganisha vijana na taasisi zinazotoa huduma hizo. Ameeleza kuwa katika kipindi cha majaribio, takribani vijana 55 walikuwa wamejisajili.

Ameongeza kuwa Mfumo wa Uratibu wa Maendeleo ya Vijana utaunganisha wizara, taasisi za umma, serikali za mitaa na wadau wengine katika kupanga, kutekeleza na kufuatilia programu za maendeleo ya vijana ili kuimarisha uwajibikaji na ushirikiano.

Aidha Waziri huyo amesema pia kutakuwa na maonyesho ya bidhaa na huduma zinazotolewa na vijana waliopata uwezeshaji, wakiwemo walioanzisha viwanda, mashamba ya umwagiliaji, biashara za samaki na walionufaika na fursa za zabuni za Serikali.

Amesema maonyesho hayo yatatoa fursa kwa vijana kupata elimu kuhusu mikopo, urasimishaji wa biashara, kodi, ununuzi wa umma, masoko na teknolojia zitakazowasaidia kuanzisha, kuendesha na kukuza shughuli zao za kiuchumi.

Nanauka amewataka vijana, taasisi na wadau wa maendeleo kushiriki maadhimisho hayo yaliyopangwa kufanyika katika ukumbi wa The Superdome, Masaki, Dar es Salaam, Novemba 23, 2026, huku akiviomba vyombo vya habari kuendelea kuelimisha jamii kuhusu fursa za maendeleo ya vijana nchini.