Dar es Salaam.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amelipongeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) kwa kuandaa TPDC Marathon 2026 iliyowezesha kukusanya zaidi ya shilingi milioni 500 kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wenye magonjwa ya moyo katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI), kiasi kilichovuka lengo la awali la shilingi milioni 200.

Akizungumza wakati wa mbio hizo zilizofanyika katika Viwanja vya Polisi Masaki jijini Dar es Salaam, leo Novemba 21, 2026, Mhe. Ndejembi amewataka wadau, wadhamini na wananchi kuendelea kuunga mkono shughuli za kijamii zinazotekelezwa kupitia michezo kwa manufaa ya makundi mbalimbali yenye uhitaji.

Amesema washiriki wa mbio hizo hawakushiriki kwa ajili ya mashindano pekee, bali walionesha uzalendo na mshikamano katika kuokoa maisha ya watoto kupitia kaulimbiu ya *“Hatua Yako, Kuokoa Maisha.”*

Aidha, amesisitiza umuhimu wa fedha zilizokusanywa kutumika kwa wakati kuwasaidia watoto wanaohitaji huduma za matibabu ya moyo ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Juma Zuberi Homera, ameipongeza TPDC kwa kuandaa mbio hizo, akieleza kuwa mchango huo unagusa moja kwa moja maisha ya watoto wenye changamoto za moyo, hususan wanaotoka katika familia zisizo na uwezo wa kumudu gharama za matibabu.

“TPDC mnaendelea kutekeleza maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha kuwa rasilimali za ndani zinatumika kurejesha manufaa kwa jamii kupitia programu mbalimbali za uwajibikaji kwa jamii, ikiwemo marathon na shughuli nyingine za CSR,” amesema Dkt. Homera.

Amesisitiza kuwa TPDC itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi chini ya usimamizi wa Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi Asilia, Dkt. James Mataragio, huku Wizara ikiendelea kusimamia utekelezaji wa maelekezo ya Serikali kwa lengo la kuimarisha sekta ya nishati nchini.

Naye Dkt. Mataragio amesema pamoja na jukumu kubwa la TPDC la kuhakikisha upatikanaji wa mafuta na gesi kwa maendeleo ya taifa, shirika hilo limeendelea kuwa mfano katika utekelezaji wa shughuli za uwajibikaji kwa jamii.

Ameipongeza TPDC kwa mchango wake katika maendeleo ya kijamii na kuyahimiza mashirika mengine yaliyo chini ya Wizara ya Nishati pamoja na taasisi nyingine za umma kuiga mfano huo kwa kuanzisha na kuendeleza programu zinazowagusa wananchi moja kwa moja.

TPDC Marathon 2026 imeendelea kuonesha nafasi ya michezo katika kuhamasisha mshikamano wa kijamii na kuchangia kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiafya, huku ikitoa matumaini kwa watoto wanaohitaji matibabu ya moyo nchini.