Afisa Biashara wa kampuni hiyo, Caroline Moshi akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam
Happy Lazaro, Dar es Salaam.
Dar es Salaam.KAMPUNI ya GSM Energies imepanga kuongeza magari mengine 500 ya kusafirishia mafuta ifikapo mwanzoni mwa mwaka 2027, hatua itakayofikisha jumla ya magari yake 800 kwa lengo la kuimarisha huduma za usambazaji wa mafuta katika sekta ya madini na maeneo mengine nchini.
Akizungumza katika maonyesho ya madini, Afisa Biashara wa kampuni hiyo, Caroline Moshi, amesema ushiriki wao katika maonyesho hayo umelenga kuitambulisha kampuni na huduma mbalimbali inazotoa, pamoja na kuonesha namna inavyoweza kushirikiana na wachimbaji na wamiliki wa migodi katika shughuli zao.
Amesema GSM Energies inatoa huduma za usambazaji na usafirishaji wa mafuta ya dizeli na petroli, ambayo ni muhimu katika kuendesha mitambo na shughuli mbalimbali za uchimbaji madini. Aidha, kampuni hiyo inatoa huduma zinazohusisha mashine nzito za kazi pamoja na vipuri vinavyotumika katika magari na mitambo ya migodini.
Moshi amesema kwa sasa GSM Energies ina magari 300 maalumu ya kusafirishia mafuta, huku GSM Truck ikiwa na magari 1,700 yanayojihusisha na usafirishaji wa mizigo mbalimbali, ikiwemo mizigo mikavu kwa kutumia magari maalumu aina ya flatbed.
Ameeleza kuwa magari ya usafirishaji wa mizigo yanafanya kazi katika nchi mbalimbali za Afrika zikiwemo Tanzania, Zambia, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Rwanda, Burundi, Malawi na Afrika Kusini, hatua inayoiwezesha kampuni kutoa huduma katika masoko ya kikanda.
Amesema magari ya GSM Energies yana mifumo ya kisasa ya ufuatiliaji wa safari kupitia teknolojia ya GPS, inayosaidia kuimarisha usalama wa mizigo, huku madereva wake wakiwa wamepatiwa mafunzo maalumu ili kuhakikisha huduma zinazotolewa zinazingatia viwango vya usalama na ubora.
Ameongeza kuwa kampuni hiyo inaendelea na ujenzi wa bohari kubwa ya mafuta Kigamboni, Dar es Salaam, yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 105, ambayo inatarajiwa kukamilika mwanzoni mwa mwaka 2027 na kuongeza uwezo wa kampuni kuhudumia wateja wake.
Moshi amewahimiza wachimbaji na wamiliki wa migodi kutumia huduma za GSM kwa kuwa kampuni hiyo imejipanga kutoa suluhisho la mahitaji mbalimbali ya sekta ya madini, kuanzia usafirishaji wa mizigo, ugavi wa mafuta hadi upatikanaji wa mashine na vipuri, akisisitiza kuwa lengo ni kuwa mshirika wa kuaminika katika kukuza shughuli za uchimbaji nchini.
