Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akiwatunuku wahitimu vyeti vya ngazi mbalimbali za taaluma wakati wa Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Duru ya Kwanza, yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya chuo hicho, jijini Dodoma

Na. Chedaiwe Msuya, Abdul Madenge, WF – Dodoma

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula, amewataka wahitimu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kutumia elimu, maarifa na ujuzi walioupata kujiajiri, kuanzisha shughuli za kiuchumi na kuajiri wengine badala ya kutegemea ajira za kuajiriwa pekee.Akiongea kwa niaba ya Mhe. Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar (Mb), katika Mahafali ya 40 ya Chuo Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Julius K. Nyerere, Kampasi Kuu ya Dodoma, Mhe. Luswetula alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi, hususan vijana, kupata elimu, mitaji, teknolojia na masoko ili washiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

“Wahitimu wanapaswa kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuwa sehemu ya suluhisho la changamoto za kiuchumi na kijamii, kwa kubuni fursa za kujiajiri na kuajiri wengine.”alisema Mhe. Luswetula

Mhe. Luswetula alieleza kuwa Serikali imeongeza bajeti ya mikopo ya elimu ya juu kutoka shilingi bilioni 916.7 mwaka 2025/2026 hadi shilingi trilioni 1.06 mwaka 2026/2027, sawa na ongezeko la asilimia 15.6, ambapo idadi ya wanufaika wa mikopo hiyo inatarajiwa kuongezeka kutoka wanafunzi 252,773 hadi 289,932.

Aidha, Serikali imetenga shilingi bilioni 9.6 kupitia Samia Scholarship kwa wanafunzi 2,738 wa fani za Sayansi, Teknolojia, Uhandisi, Hisabati na Tiba. Pia imetenga shilingi bilioni 200 kwa Programu ya Kitaifa ya Uwezeshaji Vijana Kiuchumi ili kukuza ujasiriamali na kuongeza ajira.

Mhe. Luswetula aliongeza kuwa Serikali inaendelea kutekeleza utaratibu wa kutenga asilimia 10 ya mapato ya Halmashauri kwa ajili ya mikopo kwa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu, pamoja na asilimia 30 ya manunuzi ya umma kwa makundi hayo.

Katika hatua nyingine, Mhe. Luswetula alikipongeza Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini kwa kuanzisha Kituo cha Ujasiriamali na Ubunifu (MEI), kinachowawezesha wanafunzi kubadilisha mawazo ya ubunifu kuwa bidhaa na huduma zenye tija. Alisema kituo hicho kinaunganisha elimu na mahitaji ya soko, huku kikichochea uanzishaji wa biashara na ajira.

“Ninapenda kukipongeza Chuo kupitia Kituo chake cha Ubunifu cha Ujasiriamali na Ubunifu “Mipango Entrepreneurship and Innovation (MEI) Centre” kwa jitihada kubwa za kukuza ubunifu, ujasiriamali na kuwawezesha vijana kubuni na kuendeleza mawazo bunifu yenye uwezo wa kuanzisha kuunda bidhaa na huduma mpya.” Alisema Mhe. Luswetula

Mhe. Luswetula pia alisema Serikali inaunga mkono mpango wa Chuo kufungua Kituo cha Mafunzo cha Kanda ya Nyanda za Juu Kusini mkoani Songwe ili kupanua upatikanaji wa elimu. Aliwataka wahitimu kuwa waadilifu, wenye nidhamu na uwajibikaji, huku wakiendelea kujifunza na kutumia maarifa yao kutatua changamoto za maendeleo.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini, Profesa Mayaya alisema jumla ya wanafunzi 6,076, wakiwemo wanaume 2,741 na wanawake 3,335, wamehitimu katika programu mbalimbali kuanzia Astashahada ya Msingi hadi Shahada ya Uzamili. Alisema mafunzo hayo yalihusisha nadharia na vitendo, tafiti, mafunzo kazini na ushirikishwaji wa jamii ili kuwaandaa wahitimu kukabiliana na changamoto za maendeleo.

Profesa Mayaya aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Fedha kwa kuendelea kuwekeza katika miundombinu ya Chuo, ikiwemo kukamilika kwa Jengo la Taaluma lenye ghorofa nne kupitia Mradi wa HEET, lenye uwezo wa kuhudumia watu 1,628 kwa wakati mmoja. Pia inaendelea kufadhili ujenzi wa mabweni mawili yenye uwezo wa kulaza wanafunzi 320 kila moja, katika Kampasi ya Miyuji, Dodoma, na Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa, Mwanza.

‘’Tunayo kila sababu ya kushukuru Serikali kwa mchango wake katika maendeleo ya miradi ya kuboresha miundombinu katika Chuo chetu, ikiwemo ujenzi wa Mabweni mawili ya wanafunzi, ambayo ni Bweni Namba Nne Miyuji lenye thamani ya Shilingi Bilioni 4.18 na uwezo wa kulaza wanafunzi 320 linajengwa katika Eneo la Miyuji Kaskazini,na Bweni Namba Mbili linalojegwa katika Kituo cha Mafunzo Kanda ya Ziwa, eneo la Kisesa, Wilaya ya Magu Mkoani Mwanza, ambalo limefikia hatua ya kupaua lenye thamani ya Shillingi Bilioni 3.70, na lina uwezo wa kulaza wanafunzi 320’’ alisema Profesa Mayaya.

Akizungumzia mafanikio ya chuo hicho, Profesa Mayaya, alisema Chuo kimefanikiwa kuwaendeleza wanafunzi 228 kupitia programu za ubunifu na ujasiriamali. Alieleza kuwa mwanafunzi mmoja alishinda nafasi ya pili katika shindano la Bahari Innovation Challenge kupitia biashara ya Kalinga Fresh Fish Farm na kupata shilingi milioni 29.8 pamoja na fursa nyingine za kibiashara. Aidha, Chuo kilipata shilingi milioni 68 kupitia programu ya Youth Ignite ya FUNGUO chini ya UNDP kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya kituo hicho.

Alisema Chuo kitaendelea kutoa mafunzo ya muda mrefu na mfupi, kufanya tafiti na kutoa huduma za ushauri elekezi katika mipango na usimamizi wa maendeleo ili kuunganisha taaluma na mahitaji halisi ya jamii.

Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini yamehitimisha hatua nyingine muhimu katika safari ya Chuo ya kuandaa wataalamu wenye maarifa, ujuzi na ubunifu, watakaotumia taaluma zao kujiajiri, kuajiri wengine na kuchochea maendeleo endelevu ya Taifa, sambamba na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inayolenga kujenga uchumi shindani, jumuishi na wenye tija, pamoja na kupanua fursa za kiuchumi na ajira kwa wananchi.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akizungumza katika Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Duru ya Kwanza, yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya chuo hicho, jijini Dodoma, Novemba 20, 2026.

Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Profesa Joseph Kuzilwa, akimkaribisha mgeni rasmi kuhutubia Mahafali ya 40 ya chuo hicho, Duru ya Kwanza, yaliyofanyika katika Kampasi Kuu, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb) (katikati), akiongoza maandamano ya Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Duru ya Kwanza, yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya chuo hicho, jijini Dodoma, Novemba 20, 2026. Kulia kwake ni Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la chuo hicho, Profesa Joseph Kuzilwa, na kushoto kwake ni Mkuu wa chuo hicho, Profesa Hozen Mayaya.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akikagua bweni la Hostel katika Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), wakati wa ziara yake chuoni hapo kwa ajili ya kushiriki Mahafali ya 40 ya chuo hicho, Duru ya Kwanza, jijini Dodoma.

Naibu Waziri wa Fedha, Mhe. Laurent Deogratius Luswetula (Mb), akitembelea maonesho ya shughuli mbalimbali za ujasiriamali zinazofanywa na wanafunzi wa Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), wakati wa Mahafali ya 40 ya chuo hicho, Duru ya Kwanza, yaliyofanyika katika Kampasi Kuu, jijini Dodoma.

Wahitimu wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi wakati wa Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Duru ya Kwanza, yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya chuo hicho, jijini Dodoma.

Picha mbalimbali zikionesha matukio tofauti yaliyojiri wakati wa Mahafali ya 40 ya Chuo cha Mipango ya Maendeleo Vijijini (IRDP), Duru ya Kwanza, yaliyofanyika katika Kampasi Kuu ya chuo hicho, jijini Dodoma, Novemba 20, 2026.

(Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)