Shirika la Ndege la IndiGo Air limezindua safari yake ya kwanza ya moja kwa moja kutoka Mumbai, India hadi Dar es Salaam, Tanzania. IndiGo linakuwa shirika pekee la ndege la India kutoa huduma ya usafiri wa moja kwa moja kati ya Mumbai na Dar es Salaam ikiunga mkono juhudi za shirika pekee la Tanzania (Air Tanzania) aliyoanza safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Mumbai mwaka 2019. 

Akizungumza baada ya hafla ya uzinduzi, Balozi wa Tanzania nchini India Mhe. Annisa Mbega, amesema kuanzishwa kwa safari za ndege za kila siku za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam kwenda Mumbai kunatarajiwa kuchochea zaidi biashara, uwekezaji, utalii, na mabadilishano ya kielimu kwa kuimarisha muunganisho kati ya Tanzania na India.

Balozi Mbega ameongeza kuwa India ni mmoja wa washirika wakubwa wa kibiashara wa Tanzania, kwa kuwa ushirikiano unaokua katika sekta mbalimbali ikiwemo viwanda, kilimo, na afya, Hivyo, kuzinduliwa kwa safari za ndege za kila siku za moja kwa moja kati ya Mumbai na Dar es Salaam kunasisitiza dhamira ya viongozi wetu wa Tanzania na India ya kujenga uhusiano imara zaidi. Tanzania ni mshirika muhimu wa kiuchumi kwa India na lango la kuingia Afrika Mashariki, huku kukiwa na mahitaji yanayoongezeka ya usafiri yanayochochewa na biashara, uwekezaji, utalii, na mahusiano ya kiutamaduni”.

IndiGo Air ni moja ya mashirika makubwa ya ndege ya nchini India ikiwa na ndege 440, ambazo hufanya zaidi ya safari 2,200 za ndege kila siku, zikiunganisha maeneo 141 (ambapo 45 ni ya kimataifa), na ilihudumia wateja milioni 124 mwaka uliopita (2025).