Na Mwandishi wetu– Dar es Salaam
Ubalozi wa Italia nchini Tanzania unatarajia kuadhimisha Toleo la 11 la Wiki ya Vyakula vya Kiitaliano Duniani kuanzia Novemba 23 hadi 29, 2026, kwa lengo la kutangaza utajiri wa utamaduni wa vyakula vya Italia, kuimarisha uhusiano wa kitamaduni na kukuza ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara kati ya Italia na Tanzania.
Akizungumza na waandishi wa habari katika makazi ya Balozi wa Italia jijini Dar es Salaam, Balozi wa Italia nchini Tanzania Mhe Giuseppe Coppola amesema maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika chini ya kaulimbiu isemayo “Vyakula vya Kiitaliano, Urithi wa UNESCO: Maeneo na Minyororo ya Thamani ya Ubora.”
Amesema kaulimbiu hiyo inalenga kuonesha utajiri na utofauti wa mapishi ya asili ya Italia pamoja na uhusiano uliopo kati ya vyakula, maeneo ya uzalishaji, utamaduni, jamii na ubora wa bidhaa zinazotumika katika maandalizi ya vyakula.
Ameeleza kuwa vyakula vya Kiitaliano si sehemu ya utambulisho wa kitamaduni wa nchi hiyo pekee, bali pia vinaonesha umuhimu wa kuhifadhi mila za mapishi, kuendeleza uzalishaji bora wa kilimo na kuimarisha minyororo endelevu ya thamani ya chakula.
Balozi Mhe Giuseppe Coppola amesema Wiki ya Vyakula vya Kiitaliano Duniani ni mpango wa kila mwaka unaoratibiwa na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Italia kwa msaada wa Wakala wa Biashara wa Italia (ITA/ICE), ambao unalenga kutangaza bidhaa za Italia katika masoko ya kimataifa na kuimarisha ushirikiano wa kibiashara na mataifa mbalimbali.
Amesema nchini Tanzania maadhimisho hayo yatafanyika kwa kushirikiana na migahawa ya Kiitaliano inayofanya kazi Tanzania Bara na Zanzibar, ambayo imekuwa ikichangia kutangaza mapishi halisi ya Italia na kukuza mabadilishano ya kitamaduni kati ya wananchi wa nchi hizo mbili.
Amefafanua kuwa migahawa hiyo ni daraja muhimu la kuunganisha Italia na Tanzania kupitia vyakula, utamaduni na uzoefu wa mapishi, huku ikisaidia jamii za Kitanzania kufahamu na kuthamini zaidi utamaduni wa vyakula vya Italia.
Katika hatua nyingine, amesema ushirikiano wa Italia na Tanzania hauishii katika kutangaza bidhaa za Italia pekee, bali pia unalenga kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini, kuendeleza ujuzi na kuibua fursa endelevu za kiuchumi kupitia sekta mbalimbali za uzalishaji.
Amesema Italia inaendelea kuunga mkono sekta za uzalishaji nchini Tanzania kupitia programu za Ushirikiano wa Maendeleo, ikiwemo sekta ya kahawa kwa lengo la kuimarisha uzalishaji wa ndani na mnyororo wa thamani wa zao hilo.
Kuhusu sekta ya utalii, amesema Italia inachangia katika mafunzo ya kitaaluma na maendeleo ya ujuzi katika sekta ya utalii na huduma za malazi ili kuongeza uwezo wa ndani na kuboresha ubora pamoja na ushindani wa sekta hiyo nchini Tanzania.
Amebainisha kuwa watalii kutoka Italia ni miongoni mwa vyanzo muhimu vya wageni wa kimataifa wanaotembelea Tanzania, wakiwa chanzo kikuu cha watalii wa kimataifa wanaotembelea Zanzibar na cha pili kwa ukubwa kwa Tanzania Bara.
Aidha, amesema biashara ya mazao ya kilimo na bidhaa zinazotokana na kilimo ni miongoni mwa nguzo muhimu za biashara na uwekezaji kati ya Italia na Tanzania, akitolea mfano Jukwaa la Biashara la Umoja wa Ulaya na Tanzania lililofanyika Cesena mwezi Oktoba 2026, ambako sekta hiyo ilikuwa miongoni mwa zilizojadiliwa.
Katika maadhimisho hayo, migahawa mbalimbali kutoka Dar es Salaam, Zanzibar, Arusha, Dodoma na Iringa itashiriki kwa kutoa fursa kwa wananchi kupata vyakula vya Kiitaliano na kufahamu zaidi mila na ladha za maeneo mbalimbali ya Italia. Baadhi ya migahawa hiyo ni Lido – Slipway, Zuane Restaurant, DiWine Restaurant, Mediterraneo, Bella Napoli, Mama Mia, La Capannina Zanzibar, Rocco’s Kitchen na Sipe Italian Cafeteria.
Amesema wananchi wanakaribishwa kushiriki maadhimisho hayo kuanzia Novemba 23 hadi 29, 2026 kwa kutembelea migahawa itakayoshiriki na kupata fursa ya kuonja vyakula vya Kiitaliano kupitia menyu maalumu zitakazotolewa, huku taarifa zaidi zikipatikana kupitia njia rasmi za mawasiliano za Ubalozi wa Italia nchini Tanzania.
