Mkurugenzi wa Kampuni ya Raha Energies, Anand Barchha, akitoa maelezo kuhusu huduma wanazotoa kwenye maonesho hayo jijini Dar es Saalam
Happy Lazaro, Dar es Saalam .
Dar es Saalam.Mkurugenzi wa Kampuni ya Raha Energies, Anand Barchha, amesema kampuni hiyo imeendelea kuwa mdau muhimu katika sekta ya madini nchini kwa kutoa suluhisho za nishati, vilainishi na huduma za kitaalamu zinazolenga kuongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji madini.
Amesema kampuni hiyo imekuwa ikishirikiana na wadau mbalimbali wa sekta ya madini kwa kutoa bidhaa na huduma zinazosaidia kuboresha utendaji wa mitambo, kupunguza gharama za uendeshaji na kuongeza tija katika shughuli za migodini.
Barchha amesema kupitia ushirikiano wake na wadau wa kimataifa, ikiwemo Shell, kampuni hiyo imekuwa ikitoa vilainishi vyenye ubora vinavyokidhi mahitaji ya mitambo inayotumika katika shughuli za uchimbaji na uchakataji wa madini.
Ameeleza kuwa mbali na kusambaza bidhaa za nishati na vilainishi, kampuni hiyo pia hutoa utaalamu wa kiufundi na huduma za matengenezo zinazolenga kuhakikisha mitambo ya migodini inafanya kazi kwa ufanisi na kwa muda mrefu.
Aidha, amesema Tanzania ina utajiri mkubwa wa rasilimali za madini, hivyo ni muhimu kuendelea kuweka mazingira yatakayovutia uwekezaji na kuwezesha kampuni zinazotoa huduma na teknolojia mbalimbali kushiriki katika kukuza sekta hiyo.
Amesisitiza kuwa kampuni hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya madini kutoa suluhisho endelevu za nishati, bidhaa bora na utaalamu wa kiufundi ili kusaidia kuongeza thamani ya shughuli za uchimbaji na kukuza uchumi wa nchi.
Kwa upande wake, Mshauri wa Kiufundi wa Kampuni ya Vivo Energy (Shell), Haji Kibwesi, amesema kampuni hiyo kwa kushirikiana na Prime Region, ambayo ni msambazaji wa vilainishi vya Shell chini ya leseni ya Vivo Energy, imeendelea kupanua huduma zake katika sekta ya madini nchini.
Kibwesi amesema Shell ina bidhaa mbalimbali za vilainishi zenye ubora na teknolojia inayokidhi mahitaji ya mitambo ya kisasa inayotumika migodini, huku akieleza kuwa matumizi ya vilainishi sahihi ni muhimu katika kulinda mitambo, kupunguza uchakavu wa vifaa na kuongeza ufanisi wa shughuli za uchimbaji madini.

