Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Vincent Kizenga, akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonesho hayo jijini Dar es Saaalam

Happy Lazaro, Dar es Saalam 

Dar es Saalam.Kampuni ya TAKECHARGE INTERNATIONAL imejipanga kuanzisha kiwanda cha kuzalisha vifaa vinavyotumika katika shughuli za uchakataji wa madini, ikiwa ni sehemu ya kuongeza ushiriki wa wazawa katika mnyororo wa thamani wa sekta ya madini nchini.

Akizungumza katika maonesho ya kimataifa ya madini, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Vincent Kizenga, amesema uwekezaji huo unalenga kuongeza uwezo wa ndani katika uzalishaji wa vifaa vinavyohitajika migodini na kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya nchi.

Amesema kampuni hiyo inayomilikiwa kwa asilimia 100 na Watanzania imekuwa ikijihusisha na usambazaji wa vifaa mbalimbali vya migodini ikiwemo vyuma, grinding media pamoja na huduma za kiusalama za kitaalamu kwa kushirikiana na kampuni za kimataifa.

Kizenga amesema kupitia fursa za sera ya ushiriki wa wazawa (Local Content), kampuni hiyo imeweza kupanua shughuli zake za kibiashara na kuhudumia wadau katika migodi mbalimbali ikiwemo Barrick, Sotta Mining pamoja na mradi wa Kabanga Nickel.

Amefafanua kuwa shughuli za kampuni hiyo zimekuwa zikichangia uchumi wa wananchi kupitia ajira na ushirikishwaji wa wafanyabiashara wa ndani katika upatikanaji wa vifaa vinavyotumika kwenye shughuli za uchimbaji madini.

“Ushirikiano na makampuni kutoka China, Afrika Kusini na Ghana umeiwezesha kampuni hiyo kupata teknolojia na utaalamu wa kimataifa ambao unasaidia kuwajengea uwezo Watanzania katika sekta hiyo.”amesema Kizenga .

Aidha ameishukuru Serikali kwa kuweka mazingira yanayowawezesha wazawa kushiriki katika sekta ya madini, akisema maonesho ya kimataifa ni fursa muhimu ya kuwaunganisha wafanyabiashara wa ndani na wawekezaji pamoja na kupata maarifa mapya kutoka mataifa mbalimbali.

“Naomba niwashauri Watanzania kutokuwa na hofu ya kuingia katika sekta ya madini kutokana na dhana kwamba inahitaji mitaji mikubwa na utaalamu wa hali ya juu, akisisitiza kuwa mafanikio yanaanzia kwenye uamuzi wa kuthubutu na kutumia fursa za mafunzo na ushirikiano zilizopo nchini.”amesema Kizenga